Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB
imekamilisha zoezi la kuunganisha mfumo wake mkuu wa kibenki na Bodi ya Mikopo
ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikiwa ni utekelezaji wa sehemu ya dhamira
ya benki hiyo kuimarisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanafunzi katika vyuo vikuu
kupata bidhaa za kibenki zenye hali ya juu ya usalama, ufanisi na uvumbuzi.
Akizungumza wakati wa kongamano lililofanyika jijini Dar es
Salaam jana lililoandaliwa na Bodi ya Mikopo na kuwakutanisha wadau mbalimbali
wa elimu chini, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi wa Benki ya NMB Filbert Mponzi
alisema mfumo huo kwa kiwango kikubwa umerahisisha utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Wanafunzi sasa wataweza kufurahia huduma za kibenki bila
matatizo baada ya kuunganishwa kwa mfumo mkuu wa benki ya NMB na Bodi ya
Mikopo. Muunganisho huu utahakikisha kuwa mikopo sasa inatolewa kwa wanafunzi
kwa haraka na kwa urahisi zaidi,” Mponzi alisema.
Aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kufungua akaunti na benki
yake ilikunufaika na faida lukuki zikiwemo mikopo ya papo kwa papo yenye
masharti nafuu kuanzia shilingi elfu moja hadi shilingi laki 5.
Mponzi wakati wa kongamano hilo alisisitiza dhamira ya benki
hiyo kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na taasisi za
elimunchini ili kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu kuanzia ngazi ya chini.
“Sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele vyetu muhimu. Ili
kusisitiza dhamira yetu ya kusaidia elimu ya juu, mwaka jana tulitenga mikopo
ya shilingi bilioni 200 kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kufuatia majadiliano ya
karibu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,” Mponzi alisema.
Aliongeza, “Wanafunzi wanaweza kuomba mikopo kuanzia
shilingi laki mbili hadi hadi shilingi milioni 10 kwa riba nafuu ya asilimia 9
tu,”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dk.Bill Kiwia wakati wa hafla hiyo alisema
lengo la kongamano hilo ni kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali
wanaohusika na utendaji wa utoaji wa fedha kwa taasisi yake.
Alisema kuwa bodi hiyo kwa sasa inawafikia zaidi ya
wanafunzi laki mbili wenye uhitaji lakini tayari imepanga mipango ya kuwafikia
wanafunzi wengi zaidi na kuongeza kuwa hata hivyo itategemea upatikanaji wa
rasilimali fedha.
“Hatujaridhishwa na hali ya sasa kwa sababu mahitaji ni
makubwa kuliko rasilimali zilizopo. Bado tunatafuta rasilimali fedha mbadala
ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi,” alisisitiza.
Aliwataka wanufaika wa mikopo ya bodi yake kuhakikisha
wanarejesha mikopo yao kwa wakati ili kuiwezesha taasisi yake kujiendesha kwa
ufanisi kwa manufaa ya wanafunzi wengi wenye uhitaji.




No comments:
Post a Comment