Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda (katikati) akiongoza maandamano ya wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakati wakiwasili kwenye mahafali ya 21 ya taasisi hiyo yaliyofanyika Novemba 17, 2023. Kulia kwake ni Wakili Said Chuguma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHEREHE za Mahafali ya 21 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya
Singida imemalizika huku idadi kubwa ya wanawake ikizidi kuongezeka mara dufu
ikilinganishwa na idadi ya wanaume.
Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo jumla ya wanawake 938 sawa na
asilimia 55.2 wamehitimu katika mahafali hayo Kampasi ya Singida ikilinganishwa
na idadi ya wanaume 762 sawa na asilimia 44.8.
Akizungumza kwenye mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 17, 2023 Afisa
Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William
Pallangyo alisema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1,700 katika kampasi
hiyo kati yao wanawake 938 sawa na asilimia 55.2 na wanaume 762 sawa na
asilimia 44.8, wamepata tunuku zao kwenye fani mbalimbali.
Alisema jumla ya Wahitimu ngazi ya Cheti cha Awali ni 567, Astashahada 452,
Stashahada 491, na Shahada 190.
Profesa Pallangyo alisema idadi hiyo kubwa ya wahitimu wanawake
inadhihirisha kwamba TIA inanaunga mkono jitihada za Serikali, kwa kutoa fursa
ya mafunzo pasipo ubaguzi.
Alisema idadi ya wahitimu wote wa TIA kwa mwaka wa masomo 2022/2023 kwa Kampasi za Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Singida ni 13,218 ambapo wanawake ni 7,139 sawa na asilimia 54 na wanaume ni 6,079 sawa na asilimia 46.
Alisema wanaposherehekea mahafali hayo ya Ishirini na
moja TIA imepiga hatua kubwa katika uendeshaji wa mafunzo, huduma ya ushauri wa
kitaalam, rasilimali watu, pamoja na miundombinu ya kusomea na kufundishia
katika kampasi hii ya Singida.
Alisema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa katika Kampasi ya
Singida imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Mathalani, katika mwaka huu wa
masomo 2023/2024, ulioanza Mwezi Oktoba, 2023, jumla ya wanachuo 1,443
wamedahiliwa katika kampasi ya Singida.
Aliongeza kuwa hata hivyo, zoezi la usajili bado linaendelea na lengo ni kudahili wanachuo wapya 2,600 ukilinganisha na udahili wa wanachuo 1,556 katika mwaka wa masomo 2022/2023.
Alisema ongezeko hilo la wanafunzi kwa kiasi kikubwa linatokana na mambo makubwa matatu ambayo ni ubora wa elimu itolewayo inayotokana na mitaala inayowajengea wanachuo wa ngazi zote msingi wa umahiri hivyo kumwezesha mhitimu kuajiriwa na hata kujiajiri pindi anapohitimu masomo yake. Hatua hii huwafanya wazazi na wanafunzi kuichagua TIA.
Utaratibu mzuri wa Serikali wa kuwapangia vyuo moja kwa
moja wahitimu wa kidato cha nne waliofaulu na kukidhi vigezo (kupitia
TAMISEMI). Mathalan, katika mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya wanafunzi 1,170.
"Ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada
hatua ambayo imewezesha watanzania wengi wenye sifa kumudu gharama za
masomo. Kwa mfano, katika mwaka huu
2023/2024 Serikali imepanga kuwafadhili wanachuo 810
wa shahada katika kampasi hii ya Singida na hili ni ongezeko la asilimia 15.9
ukilinganisha na wanachuo 699
waliofadhiliwa mwaka 2022/2023," alisema Pallangyo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter ambaye alikuwa mgeni
rasmi kwenye mahafali hayo alisema amefurahishwa sana na mpango
wa ukuzaji na uendelezaji wa wanafunzi kitaaluma na kitaalamu yaani (Career
Development Program) wanaoufanya kwa wanafunzi wa taasisi hiyo kwa kujitengenezea
fursa muhimu za kibiashara kwa kuendeleza
ubunifu wao ambao ni fursa adhimu kwa wanafunzi hao.
“ Mmedhihirisha umahiri wenu, na kutupa wasaa wa kushuhudia matunda ya juhudi zenu. Hivyo, sina budi kwa niaba ya Serikali, kutoa pongezi zangu za dhati kwa Uongozi, Wahadhiri na wafanyakazi Waendeshaji, kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha mafunzo yenu.
Safari yenu ya mafunzo haikuwa nyepesi; safari yenu ilihitaji uvumilivu, ushirikiano, nidhamu, kujituma na zaidi ya yote kumtegemea Mungu. Kwa pamoja, haya ndiyo yamewawezesha kufikia hatua hii muhimu,” Mwenda alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Serikali.
Aidha, Mwenda aliwaasa wahitimu hao kwamba, hatua
waliyoifikia iwe ni chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma
ili kuweza kushindana katika soko la ajira na kujiajiri na kuwa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan inahimiza sana Taasisi zote kuhakikisha elimu
inayotolewa kwa wanafunzi iwe elimu, ujuzi na maarifa ya kukidhi mahitaji ya
soko ili itumike kuleta tija na maendeleo yanayoendana na mabadiliko ya Sayansi
na Teknolojia.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo, akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema akiwatambulisha wageni waalikwa.
Mhitimu wa Shahada ya Uhasibu kutoka kampasi ya Singida, Patrick Edward akipokea cheti kutoka kwa mgeni rasmi
Mratibu wa Taaluma, Flora Lemnge akizungumza.
Viongozi wakiwa meza kuu. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha, Thabiti Dokodoko, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Wakili Said Chiguma, Mgeni rasmi wa Mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Afisa Mtendaji wa TIA, Profesa, William Pallangyo na Mkurugenzi wa TIA, Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema.
Wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wakiwa kwenye maandamano kuelekea kwenye viwanja vya mahafali hayo.
Wahitimu wa Shahada ya Uhasibu wakionesha furaha yao kabla ya kutunukiwa vyeti vyao.
Viongozi mbalimbali na Waadhiri wa TIA wakiwa wamejipanga foleni tayari kwa kumpokea mgeni rasmi wa mahafali hayo.
Mratibu wa Ujasiriamali na Kituo Atamizi wa Kampasi ya Singida, Mohamed Kaluse, akizungumza kwenye mahafali hayo ya 21.
Wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wakionesha furaha zao baada ya kutunukiwa vyeti vyao.

No comments:
Post a Comment