WANANCHI SINGIDA WATOA KONGOLE KWA MO DEWJI FOUNDATION, SHIRIKA LA ESTL UFUFUAJI VISIMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 6 November 2023

WANANCHI SINGIDA WATOA KONGOLE KWA MO DEWJI FOUNDATION, SHIRIKA LA ESTL UFUFUAJI VISIMA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la Kiserikali la  Empower Society Transform Lives (ESTL), ambalo linasimamia ufufuaji wa visima vilivyochimbwa na Mohammed Dewji Jimbo la Singida Mjini, alipokuwa Mbunge, Joshua Ntandu akiwa na Mwakilishi wa Taasisi ya Mo Dewji Foundation, Janeth Mashauri wakati walipotembelea kisima kilichopo Kitongoji cha Ntunduu Kata ya Unyamikumbi  Novemba 2, 2023 baada ya kufufuliwa.

Na Dotto Mwaibale, Singida

WANANCHI wa Manispaa ya Singida wameipongeza Taasisi  ya MO Dewji Foundation na Shirika lisilo la Kiserikali la  Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na kubadili maisha ya jamii baada ya kufufua visima 19 vya maji safi na salama vilivyo jengwa na Mohammed Dewji wakati alipokuwa Mbunge wa Jimbo la Singida mjini.

Wananchi waliotoa pongezi hizo ni kutoka katika kata ya Unyambwa, Unyianga, Mtamaa na Unyamikumbi ambazo zipo katika Manispaa ya Singida.

Akizungumza wakati wa zoezi la ufufuaji wa visima hivyo lililofanyika Novemba 2, 2023 katika kata hizo na kupata maoni ya wananchi , Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo ambalo linasimamia ufufuaji wa visima hivyo , Joshua Ntandu alisema jumla ya Sh. Milioni 119 zimetumika kufanya kazi hiyo.

“Lengo letu lilikuwa ni kuona kama visima vilivyochimbwa awali je vinaweza kufanya kazi na ndipo tuone kama kutakuwa na uhitaji mkubwa wa maji na ninyi sasa mje na mapendekezo ya visima hivyo vichimbwe maeneo gani na vitatumia nishati ipi kwa ajili ya kuyasukuma kama ni umeme wa jua au wa Tanesco na njia nyingine,” alisema Ntandu.

Alisema mpango wa ufufuaji wa visima hivyo ulikuwa ni wa muda mfupi lakini lengo lao ni kutaka kuona mkoa mzima wa Singida unapata maji safi na salama na yapatikane umbali usiozidi mita 400 kuanzia watu walipo.

Ntandu alihimiza umuhimu wa kuvitunza visima hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kutengeneza mpango mzuri utakaotumika kuvifanyia matengenezo vitakapokuwa na changamoto ya kuharibika kwa kuwa wao hawatahusika tena na matengenezo hayo.

Mhandisi wa Maji wa Shirika hilo, Edward Barnaba alisema baada ya kufanya upembuzi yakinifu wa visima vyote 38  vilivyo chimbwa na Dewji ni visima hivyo 19 pekee ndivyo vilivyoonekana kuwa vinaweza kufufuliwa na kurudi katika hali yake ya kawaida ambavyo vitakamilika mapema mwezi huu wa Novemba.

Barnaba alisema visima hivyo vinaharibika kutokana na kuingia kwa mchanga na watoto kuweka mawe kwenye pampu ya kusukuma maji na kuharibu mfumo wake ambapo alishauri jirani na maeneo vilipochimbwa iachwe nafasi ya mita 60 na kuzungushiwa uzio ili mazingira yake yasiharibiwe.

Kwa upande wake Fundi Sanifu Mkuu Ubora wa Maji, Maabara ya Singida, Shifaya Munisi alisema baada ya kupima ubora wa maji baada ya kufufuliwa kwa visima hivyo yameonekana kuwa ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Mwakilishi wa Mo Dewji katika ufufuaji wa visima hivyo , Janeth Mashauri, aliwataka wananchi ambao visima vyao vimefufuliwa wavitunze kwani ni mali yao.

“Mo Dewji kazi aliyoifanya ni kuvifufua visima hivi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ombi langu kwao ni wavitunze na kurekebisha miundombinu yake itakapo haribika,” alisema Mashauri.

Mkazi wa Kitongoji cha Sanga Kata ya Unyambwa, Mwajuma  Mohamed alizishukuru taasisi hizo kwa kufufua visima hivyo na kueleza kuwa licha ya kufufuliwa bado kunachangamoto ya upatikanaji wa maji hasa kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa kitongoji hicho ambapo aliomba kama utakuwepo uwekano wachimbiwe visima vingine.

“Tunachangamoto kubwa ya maji tunatoka saa tisa usiku kuja hapa kufuata maji na tunahatarisha maisha yetu kwa kushambuliwa na fisi ni kweli maji tunapata lakini hayatutoshelezi kwani wakati kinachimbwa kisima hiki watu walikuwa wachache wasiozidi 200 lakini leo tupo zaidi ya 1500,” alisema Mwajuma.

Wananchi wengine waliozishukuru taasisi hizo kwa kufufua visima hivyo na kuomba visima zaidi viongezwe ili kusaidia  kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji ni Anifa Mkotya, Rehema Nasoro na Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Sanga, Ongoza Samwaja.

Diwani wa Kata ya Unyambwa, Shabani Magwe, Diwani wa Kata ya Mtamaa, Gwae Mbua, Diwani wa Kata ya Unyianga, Geofrey Mdama na Diwani wa Kata ya Unyamikumbi, Kipandwa Ipini wakizungumza kwa nyakati tofauti walizishukuru taasisi hizo kwa kuwakomboa wananchi na kuwaondolea adha ya kupata maji.

Madiwani hao waliziomba taasisi hizo ikiwezekana ziwachimbie visima vingine ili kukabiliana na changamoto ya maji kutokana na ongezeko la watu kwani wakati visima hivyo vilipokuwa vinachimbwa mwaka 2008 na sasa ni miaka 13 imepita katika maeneo yao kulikuwa na watu wachache.

Viongozi wa Taasisi hizo wakiwa na Diwani wa Kata ya Unyamikumbi, Kipandwa Ipini wakati walipotembelea kisima hicho.

Mhandisi wa Maji wa Shirika la ESTL, Edward Barnaba, akizungumzia zoezi zima la ufufuaji wa visima hivyo.

Fundi Sanifu Mkuu Ubora wa Maji, Maabara ya Singida, Shifaya Munisi , akizungumzia ubora wa maji ya visima hivyo.

Diwani wa Kata ya Unyambwa, Shabani Magwe, akitoa shukurani kwa taasisi hizo kwa kufufua visima hivyo.

Diwani wa Kata ya Unyamikumbi, Kipandwa Ipini, akizungumzia visima hivyo.

Diwani wa Kata ya Mtamaa, Gwae Mbua, akizungumza na kutoa shukurani kwa taasisi hizo kwa kufufua visima hivyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Unyamikumbi A, Juma Ngowi akizungumza. 

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la ESTL, Joshua Ntandu, mmoja wa wananchi wa Kata ya Mtamaha wakati walipotembelea kisima kilichofufuliwa katika Kitongoji cha Mnyituka.  

Wananchi wakichota maji katika kisima kilichofufuliwa kitongoji cha Mangua Mitogho.


Wanawake wakichota maji katika Kisima kilichofufuliwa eneo la Sanga Kata ya Unyambwa.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Unyambwa, Samson Kimu, akizungumza.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sanga, Iddi Nkungu akichangia jambo katika mkutano huo.

Wanawake wa Kitongoji cha Sanga wakiwa katika mkutano huo.

Anifa Mkotya akishukuru kwa kufufuliwa visima hivyo.

Mwajuma Mohamed akizungumzia changamoto ya maji katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa kitongoji cha Sanga.

Afisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Shirika la ESTL, Masifia Yeremia Yohana, akielekeza jambo wakati wa kutembelea kisima kilichofufuliwa kitongoji cha Sanga.

Bibi Miriam Abdallah (75) akichota maji katika kisima kilichofufuliwa Kitongoji cha Munyituka kilichopo Kata ya Mtamaa.

Wananchi wa Kata ya Unyianga A eneo la Isenge wakisubiri kutoa shukurani zao kwa viongozi wa taasisi hizo baada ya kufufuliwa katika kisima.

Diwani wa Kata ya Unyianga, Geofrey Mdama (kulia) akiwa na viongozi wengine katika Kisima kilichofufuliwa katika eneo la Isenge.

Wananchi wa Kitongoji cha Ntunduu Kata ya Unyamikumbi wakiangalia maji yaliyokuwa yakitoka katika kisima kilichofufuliwa eneo hilo.


Muonekano wa gari lenye mitambo ya kufufulia visima hivyo likiwa kazini Kata ya Unyamikumbi.


Watoto wakishuhudia maji yakitoka katika eneo hilo la Ntunduu.

No comments:

Post a Comment