Wajumbe wa mkutano wa ushirikiano kati ya SJMT na SMZ katika sekta ya ujenzi wakifuatilia majadiliano ya mkutano wa sita unaofanyika jijini Mwanza. |
KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Mhandisi Mussa Kashinde amezungumzia umuhimu wa wajumbe wa Mkutano wa sita wa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika sekta ya ujenzi kushiriki kikamilifu kwenye mkutano wa kubadilisha uzoefu na kujengeana uwezo ili kuleta tija kwa pande zote za muungano.
Akizungumza jijini Mwanza wakati akifungua mkutano huo ngazi ya wataalam Mhandisi Kashinde amewataka wataalam hao kuibua hoja na kuzipatia ufumbuzi ili kuleta maendeleo endelevu kwa sekta ya ujenzi.
Mkutano huo ambao ni muendelezo wa makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi zilizopo chini ya Wizara Ujenzi Tanzania Bara na Wizara Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Tanzania Visiwani unajumuisha taasisi za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo, Wahandisi na Wakadiriaji Majenzi (AEQSRB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).
“Mkutano huu ni muhimu na ni muendelezo wa mkutano wa tano uliofanyika mwaka jana Zanzibar wa makubaliano kati ya SJMT na SMZ katika sekta ya Ujenzi, hivyo ni vyema wajumbe kutoka pande zote mbili kushiriki kwa ukamilifu”, amesisitiza Mhandisi Kashinde.
Wajumbe kutoka pande zote mbili wameonesha umuhimu wa ushrikano katika kuendeleza na kuimarisha sekta hiyo ikiwemo usimamizi wa programu zinazohusu wahitimu wa taaluma ya uhandisi nchini na uhamasishaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wanawake ili kuongeza idadi yao.
Makubaliano ya ushirikiano yanalenga kubadilishana utaalamu katika maeneo ya kiufundi na kiutawala, kuratibu utambuzi wa pande zote mbili katika usajili wa wahandisi, wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi pamoja na kushirikiana katika mipango ya maendeleo ya kitaalamu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI
No comments:
Post a Comment