| Meneja Mradi wa Kampuni ya Sinohydro, Guo Kun
akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa alipotembelea mradi huo leo jijini Dar es Salaam. |
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuanzia sasa kutowapa kazi wakandarasi wote wanaochelewesha miradi ya ujenzi na
menejimenti zao kufikishwa ofisini kwake mara moja kwa hatua zaidi.
Amewataka wasimamizi wa miradi ya barabara kuwa wabunifu na kusimamia majukumu yao kikamilifu ili kuondoa changamoto ndogondogo kwa watumiaji wa miundombinu ya ujenzi wa barabara nchini.
Bashungwa amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati
wa ziara yake ya kukagua athari za mvua, mradi wa mabasi yaendayo kasi awamu ya
tatu na miradi mingine ya ujenzi inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema atakuwa mkali kwa watendaji au wakandarasi wazembe wanaoshindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusababisha miradi kusuasua.
Ameonya tabia ya baadhi ya wakandarasi kujenga miradi mingi kwa wakati mmoja na yote kutokuwa kwenye kasi inayotakiwa kimkataba.
"..Serikali inapotia fedha inahitaji huduma kwa haraka hivyo mameneja nchini kote hakikisheni miradi inakamilika kwa wakati", amesisitiza Waziri Bashungwa.
Aidha amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuvamia hifadhi za barabara kinyume cha sheria na kufanya biashara hali inayosababisha usumbufu na usalama hafifu kwa watumiaji wa barabara.
Aliongeza, "hifadhi ya barabara iko kwenye
sheria tangu mwaka 1932 hivyo TANROADS na TARURA isimamieni kikamilifu sheria
hiyo", amesisitiza Bashungwa.
Ametoa wito kwa wakandarasi wazawa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija na kuliwezesha Serikali kuwaamini na kuwapa miradi mingi ili kukuza uchumi wa watanzania.
Ameitaka bodi ya ushauri ya Tanroads kukutana mara moja ili kuidhinisha ujenzi wa miradi mipya ya barabara.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Dorothy Mtenga
amesema ujenzi wa BRT III unaotekelezwa
na Mkandarasi Sinohydro unatarajia
kukamilila mwezi Machi 2024.
"Tumepokea maelekezo yote yaliyotolewa na
Serikali tutaendelea kumsimamia mkandarasi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama
Serikali inavyotaka katika mradi huo wa BRT awamu ya tatu.
Alikiri kuwa ujenzi wa mradi huo upo nyuma
kimkataba ambapo sasa uko asilimia 20 wakati ulitakiwa kuwa asilimia 46.
Meneja Mradi wa Kampuni ya Sinohydro, Guo Kun
aliahidi kumaliza ujenzi kwa wakati kwani watakuwa wanafanyakazi usiku na
mchana.
Kuhusu kupunguza changamoto kwa wananchi wakati wa
ujenzi wa mradi huo alieleza kuwa mkakati wa kampuni yake ni kujenga zaidi
usiku kuliko mchana.
Imetolewa
na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi.

No comments:
Post a Comment