UJENZI WA RELI YA KISASA KIPANDE CHA MAKUTOPORA MPAKA TABORA KINAENDELEA VIZURI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 7 October 2023

UJENZI WA RELI YA KISASA KIPANDE CHA MAKUTOPORA MPAKA TABORA KINAENDELEA VIZURI

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Waandishi wa Habari, mara baada ya kukagua Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tatu Makutopora Mkoani Singida mpaka Tabora  kilometa 368.

Kazi ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tatu Makutopora Mkoani Singida mpaka Tabora  kilometa 368 unaendelea.

WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa  amesema kuwa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tatu Makutopora Mkoani Singida mpaka Tabora  kilometa 368 unaendelea vizuri japo kunachangamoto mbalimbali . 

Waziri Mbarawa ameyasema hayo leo alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo ambapo amesisitiza kuwa licha ya changamoto zilizobainika bado  serikali itahakikisha changamoto hizo zinatatuliwa na mradi unakamilika kwa wakati.

"Kasi ya ujenzi tuliyoitarajia imepungua,leo hii tulitakiwa kufikia asilimia ishirini na mbili lakini leo tumefikia asilimia kumi na mbili kuna asilimia kumi zimepungua hii ni changamoto lakini tukiweka mikakati vizuri tunaweza kulitatua," amesema Prof. Mbarawa.

Aidha Mbarawa amesema kuwa hakuna taarifa yoyote kwamba mkandarasi ameshindwa kuendelea na mradi kwani kazi bado inaendelea huku akionyesha ushahidi wa kazi zinavyoendelea katika kituo cha Tabora ambapo ujenzi wa tuta unaendelea.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Senzige Kisenge amesema kutokana na changamoto iliyobainika TRC imemuelekeza mkandarasi kuandika mpango wa namna atakavyofidia muda uliopotea kama sehemu ya kutatua changamoto hiyo ili mradi ukamilike kwa wakati.

Mhandisi Kisenge amesema kama waziri alivyoelekeza kufanyika kikao na mkandarasi huyo huku kikao kikiongozwa na waziri ili kuhakikisha kila kitu kinawekwa sawasawa na kazi inafanikiwa.

Meneja Mradi wa ujenzi wa SGR kipande cha Makutupola - Tabora Mhandisi Edwin Ntahondi amesema hatua inayoendelea kwa sasa ni ujenzi wa tuta kuu ambapo katika kilomita 368 za mradi mkandarasi amegawanya ujenzi huo katika maeneo matano na yote yana watu wanaoendelea na kazi hiyo.


No comments:

Post a Comment