NAIBU WAZIRI CHANDE AKAGUA MIRADI MIPYA CHUO CHA UHASIBU -IAA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 30 September 2023

NAIBU WAZIRI CHANDE AKAGUA MIRADI MIPYA CHUO CHA UHASIBU -IAA

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (katikati), akikagua ujenzi wa hosteli katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa miradi inayoendelea katika chuo hicho, jijini Arusha. 


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa mhandisi wa majengo wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa miradi inayoendelea katika Chuo hicho, jijini Arusha. Wa pili kulia ni Naibu Mkuu wa Chuo anayesimamia Mipango, Fedha na Utawala, Dkt. Cairo Mwaitete na watatu kushoto ni Mbunge wa Arusha mjini, Mhe. Mrisho Gambo.



Na. Joseph Mahumi, WF, Arusha

 Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameupongeza uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa matumizi na usimamizi nzuri wa fedha za miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Chuo hicho ambayo amesema imejengwa kwa viwango vinavyolingana na thamani ya fedha iliyotumika.

 

Mhe. Chande alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa miradi inayoendelea katika Chuo hicho ukiwemo ujenzi wa jengo la Postgraduate na Hosteli, inayotekelezwa kupitia mfumo wa "force account".

 

"Hapa nimeona si thamani ya Fedha tu kwenye hii miradi, bali zaidi ya thamani ya fedha; nawapongeza sana IAA kwa kazi nzuri mnayofanya, tumeona jengo lililojengwa kwa bilioni 1.9 ambalo katika maeneo mengine jengo kama hilo limejengwa kwa gharama kubwa zaidi," alisema Mhe. Chande.

 

Alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha inatarajia kutoa jumla ya shilingi bilioni moja kwa ajili kuendeleza jitahada za ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Uhasibu Arusha.

 

Aidha, katika kuunga mkono jitihada za IAA kwenye uboreshaji wa miundombinu, Mhe. Chande aliahidi kujenga kisima cha Maji cha kisasa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya Maji.

 

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo hicho anayesimamia Mipango, Fedha na Utawala, Dkt. Cairo Mwaitete, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiwezesha IAA kutekeleza mipango yake na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

 

Aliongeza kuwa Fedha zote zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali pamoja na zinazopatikana kwa mapato ya ndani zitasimamiwa vema na zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta tija na matokeo chanya.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Felician Mtahengerwa, alisema kuwa Chuo cha Uhasibu Arusha, kimekuwa mfano bora na wa kuigwa kwenye matumizi ya mfumo wa "force account" katika ujenzi wa miradi hususani kwenye matumizi na usimamizi mzuri wa fedha, ukamilishaji wa miradi kwa wakati na thamani ya fedha kwenye miradi husika.

 

No comments:

Post a Comment