Naibu Waziri wa Ujenzi
Eng. Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo kwa wananchi wa kata ya Kalya
alipozungumza nao alipokagua maendeleo ya uanzishwaji wa barabara ya
Simbo-Kalya KM 235 mkoani Kigoma.
Mbunge wa Kigoma
Kusini Mhe. Nashon Bidyanguze akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Eng.
Godfrey Kasekenya alipokagua barabara ya Simbo-Kalya KM 235 mkoani Kigoma. |
SERIKALI imesema katika mkakati wake wa kuufungua mwambao wa ziwa Tanganyika itajenga madaraja ya Malagarasi-Ilagala na Lugonesi ili kuunganisha kwa njia fupi mikoa ya Kigoma na Katavi na hivyo kuchochea shughuli za uzalishaji wa mazao, uvuvi na ufugaji katika maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya alipokagua maendeleo ya
uanzishwaji wa barabara mpya ya Simbo-Kalya
KM 235 inayopita pembezoni mwa ziwa Tanganyika na kuunganisha mikoa ya
Kigoma na Katavi.
“ Hadi mwezi Disemba
tutahakikisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika ili kazi ya
ujenzi wa madaraja haya mawili pamoja na barabara unganishi zenye zaidi ya KM 7
uanze”, amesema Eng. Kasekenya.
Amebainisha kuwa
wakati Serikali ikitafuta fedha za kuijenga barabara hiyo itahakikisha maeneo
korofi yanajengwa kwa kiwango cha zege ili kuiwezesha kupitika kipindi chote
cha mwaka.
Naibu Waziri huyo
amewapongeza mameneja wa Wakala wa Barabara TANROADS mkoa wa Kigoma na Katavi
kwa kazi za kuanzisha barabara mpya katika maeneo yao ili kurahisisha huduma ya
usafiri ikiwa ni pamoja na kuunganisha barabara na bandari za ziwa Tanganyika.
“Kwa kweli nimeridhika kwa bidii na ubunifu wa
mameneja hawa ya kuanzisha barabara mpya huu ni ubunifu mzuri na Serikali
itatafuta fedha ili barabara hizi zijengwe kwa lami”, amesisitiza Eng.
Kasekenya.
Naibu Waziri huyo
amewataka wananchi wa mikoa ya Kigoma na Katavi kulinda miundombinu ya barabara
ili idumu kwa muda mrefu na kuepusha hasara kwa serikali na ukosefu wa usalama
kwa wananchi wanaotumia barabara hizo.
“Acheni kuchimba
mchanga barabarani na chini ya madaraja, epukeni wizi wa alama za barabarani na
taa, eleweni Serikali inatumia gharama kubwa kujenga miundombinu hii hivyo
kuilinda ni kuiunga mkono Serikali”, amesisitiza Eng. Kasekenya.
Meneja wa (TANROADS),
mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma amesema ujenzi wa barabara na madaraja
utaendana na utoaji elimu ya uzalendo kwa wananchi namna ya kuilinda
miundombinu kwa maslahi mapana ya taifa.
No comments:
Post a Comment