Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa Kampuni ya Avic wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma yenye jumla ya urefu wa kilometa 112.3; sehemu ya Ihumwa Dry Port - Matumbulu - Nala (km 60), |
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mkandarasi Avic anayejenga barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma, yenye urefu wa Kilometa 112.3 sehemu ya Ihumwa Dry Port - Matumbulu - Nala (km 60), kuhakikisha anakamilisha barabara hiyo ifikapo mwezi Desemba, 2024.
Bashungwa ametoa
agizo hilo Septemba 29, 2023, jijini Dodoma wakati akikagua maendeleo ya ujenzi
wa barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amemsisitiza mkandarasi huyo
kuongeza spidi kwenye ujenzi wa madaraja mawili ambayo yanaonekana kuchelewa
ujenzi wake.
“Sipepesi macho
kwenye usimamizi wa mikataba, kufanya kazi kwa ubora na kasi ndio kipimo chako,
ukizembea kwenye kazi hii usahau kupewa kazi nyingine za ujenzi kwenye Sekta
hii nchini”, amesema Bashungwa.
Ameahidi kutembelea
tena mradi huo ifikapo Desemba mwaka huu ili kuona uetekelezaji wa maagizo yake
na kumsisitiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana ili uweze
kukamilika kwa wakati kulingana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Aidha, Bashungwa
ameuagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kushirikiana na Shirika la
Reli (TRC), kurudisha haraka mawasiliano ya barabara ya lami eneo la Mkonze na
Nala ambalo lilibomolewa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya SGR kwani wananchi
wamekuwa wakipata kero kutokana na changamoto katika maeneo hayo.
Bashungwa amewataka
wakandarasi nchini wanaotekeleza miradi ya ujenzi kuhakikisha wanatekeleza
miradi hiyo kwa mujibu wa Mkataba na kusisitiza kutokuwa na huruma kwa yeyote
atakayekiuka mikataba hiyo.
Bashungwa amemuagiza
Mhandisi Mshauri Mzawa wa kampuni ya Inter-Consult kumsimamia mkandarasi wa
kampuni ya China Civil Engineering Corporation (CCEC) anayetekeleza sehemu ya
Nala - Veyula - Mtumba (km 52.3), kutoa vifaa vya usalama kwa wafanyakazi wake
ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea maeneo ya kazi.
Katika hatua
nyingine, Bashungwa amewaagiza Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini
kuhakikisha wanazibua mifereji ya barabara zilizo chini ya Wakala huo kabla ya
mvua hazijaanza ili zisiwe chanzo cha kuleta mafuriko, sambamba na hilo Waziri
huyo amempongeza Meneja wa TANRODS Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanya
matengenezo na kuzibua barabara na mifereji katika mkoa huo.
Kwa upande wake,
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta ameeleza kuwa mpaka sasa sehemu
ya mradi kutoka Nala – Veyula – Mtumba (km 52.3) umefika asilimia 54.3 na
sehemu inayoanzia Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala umefika asilimia 50 na sasa
wakandarasi wanaendelea na kazi mbalimbali za ujenzi wa makalavati na madaraja
makubwa mawili.
Mradi
wa Barabara ya Mzunguko wa nje ya Dodoma (Km 112.3), unagharimiwa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi Bilioni 221 na unatarajiwa
kukamilika mwezi Desemba 2024.
No comments:
Post a Comment