Na Eleuteri Mangi,
WUSM, Dar es Salaam
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema haikuwa kazi rahisi kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kushinda zabuni ya kuandaa Fainali za Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Dkt. Ndumbaro amesema
hayo Septemba 29, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye mkutano na
waandishi wa Habari kuhusu nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa
mashindano hayo makubwa barani Afrika.
“Haikuwa kazi ndogo,
ilikuwa kazi ngumu sana, tuliweka mikakati ya pamoja ya kutosha kuhakikisha
zabuni yetu ambayo sasa ni EA Pamoja AFCON 2027 inashinda. Mipango yetu ilikuwa
na nguvu na msukumo wa Marais wetu watatu; Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhe.
Dkt. William Samoye Ruto na Mhe. Jenerali Yoweri Kaguta Museveni utayari na mchango
wao kwenye mashindano haya kwetu ulikuwa mtaji wa kwanza” amesema Dkt.
Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro amesema
Wizara itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kujenga viwanja vipya viwili na
kusisitiza maandalizi mengine yafanyike haraka na kwa wakati ili Watanzania
wanufaike.
Vigezo ambavyo
vimetumika kushinda zabubi hiyo ni pamoja na Serikali zote tatu ziwe na dhamana
ya Dola za Marekani Milioni 30 kwa kila nchi ambapo jumla yake ni Dola za
Marekani Milioni 90, viwanja sita vya mashindano na kila nchi inapaswa kuwa na
angalau viwanja viwili ambapo kwa Tanzania upo Uwanja wa Benjamin Mkapa
umekidhi sifa na unaendelea kufanyiwa ukarabati wa awamu ya kwanza, Uwanja wa
Aman Zanzibar, huu unaendelea na maboresho huku Uwanja mpya wa Arusha
unatarajiwa kujengwa na kukamilika kabla ya mashindano ya AFCON 2027.
Kwa upande wake Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Bw. Wallace Karia amesema anawashukuru
mawaziri wote wa michezo, Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro, Waziri wa Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Tanzania, Mhe. Ababu Namwamba, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Kenya na Mhe. Peter Ogwang, Waziri wa Nchi Elimu na Michezo, Uganda
kwa kazi kubwa waliyoifanya kufanikisha ushindi huo nan chi hizo kupewa dhamana
ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027.
No comments:
Post a Comment