Muonekano wa barabara ya Tabora-Mambali –Bukene-Itobo inayojengwa kwa kiwango cha lami. |
NAIBU Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha maeneo korofi, mitaro na madaraja katika barabara kuu na za mikoa nchini kote yanasafisha na kuimarishwa ili kukabiliana changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Tabora-Mambali-Bukene ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea katika maeneo korofi wakati wa mvua Naibu Waziri Kasekenya amesisitiza umuhimu wa wajenzi na wasimamizi wa barabara kufuatilia na kufanyia kazi taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA).
“Habari zinasema mvua za vuli zinatarajiwa kunyesha katika kiwango cha juu ya wastani hivyo ili kuepuka mafuriko, kukatika kwa barabara na madaraja ni vema kila meneja katika mkoa wake akajipanga mapema kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza ili kutoathiri huduma za usafiri na uchukuzi”, amesema Eng. Kasekenya.
Kwa mujibu wa TMA kati ya mwezi Oktoba hadi Disemba maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita,Mwanza, Shinyanga, Simiyu,Kigoma, Dar es salaam, Pwani, Morogoro na Tanga yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani na wastani.
“Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani hivyo umakini na utayari wa kukabiliana na mvua hizo pale zitakapoleta madhara kwenye miundombinu unahitajika ili kuondoa usumbufu kwa wasafiri”, amesisitiza naibu waziri huyo wa ujenzi.
Ameonya tabia ya baadhi ya wananchi kuiba alama na taa za barabarani mkoani Tabora na kuitaka TANROADS kushirikiana kwa karibu na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kudhibniti wimbi hilo la uharibifu wa alama za barabarani mkoani Tabora hali inayoweza kusababisha ajali na kudunisha kasi ya serikali ya kupendezesha barabara.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya ametoa siku 14 kwa Mtendaji mkuu wa TEMESA kufuatilia ukarabati wa karakana ya TEMESA mkoani Tabora ili kujiridhisha kama unakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya kuboresha karakana hizo nchini.
“Tunataka karakana za TEMESA ziwe za kisasa kimuonekano na kwa huduma zinazotolewa ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya sita”, amesema Eng. Kasekenya.
Kaimu meneja wa TANROADS mkoa wa Tabora Eng. Christephola Nichombe amesema mkoa huo unaendelea na kampeni ya kuhakikisha barabara zake zinapitika wakati wote wa mwaka na sasa maeneo korofi yanaendelea kukarabatiwa.
Naibu Waziri huyo wa Ujenzi yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI.
No comments:
Post a Comment