TAARIFA YA UWASILISHAJI WA MAJUKUMU YA IDARA YA NGOs KWA KAMATI YA BUNGE YA USTAWI NA AMENDELEO YA JAMII - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 22 August 2023

TAARIFA YA UWASILISHAJI WA MAJUKUMU YA IDARA YA NGOs KWA KAMATI YA BUNGE YA USTAWI NA AMENDELEO YA JAMII

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akijibu hoja mbalimbali za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kikao kilichofanyika Agosti 22, 2023 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao kilichofanyika Agosti 22, 2023 jijini Dodoma.

Na WMJJWM Dodoma 

SERIKALI imesema uanzishaji wa Mfumo wa ramani ya utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali itasaidia kutatua  changamoto za upatikanaji wa taarifa muhimu kwa Umma kuhusu Mashirika hayo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Dkt Dorothy Gwajima ameyasema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao na Kamati hiyo Agosti 22, 2023 jijini Dodoma.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Mfumo huo utawezesha wananchi na wadau kufuatilia na kujua namna Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanavyofanya kazi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao na kwa namna gani wanaweza kupata fursa ya kunufainika na miradi hiyo.

"Nimeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kuratibu na kuzileta NGOs pamoja kwenye majadiliano ya jinsi gani kuimarisha uelewa wa jamii kwenye utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambapo pia Wahe. Wabunge watapata  fursa ya kujenga uelewa kwa upana zaidi" amesema Dkt. Gwajima.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt John Jingu amesema Wizara kwa mwaka huu imesajili na kuratibu jumla ya Mashirika 9687, kati yao Mashirika ya kimataifa ni 578, Mashirika ya Kitaifa 8001, Mashirika ya kimkoa 464 na Mashirika ya kiwilaya 647. Mashirika hayo yanatekeleza afua mbalimbali katika maeneo tofauti nchini.

Dkt. Jingu ameongeza kuwa Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs inafanya mafunzo mbalimbali kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuwapa elimu hiyo kwa kufuata taratibu na Sheria zilizopo.

Wizara kwa kushirikiana na Wasajili wasaidizi katika Mikoa na Halmashauri nchini wamefuatilia jumla ya Mashirika 2663 ambayo ni zaidi ya asilimia 100 ya Mashirika yaliyopanga kufikiwa.

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya masuala kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vickness Mayao amesema mfumo wa ramani ya kidigitali utatambua afua mbalimbali zinazofanywa na Mashirika yaliyopo nchini ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za Mashirika yaliyopo na afua zinazotekelezwa.

Ameongeza kuwa suala la msamaha wa Kodi kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni ajenda ambayo imeibuka katika Majukwaa ya NGOs yanayoendelea kufanyika kwenye ngazi ya Mikoa ila Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wadau kwa mikoa kupitia Kitabu cha Mwongozo wa kuomba msaada wa Kodi kwa Mashirika hayo.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Mariam Kisangi  ameipongeza Wizara kwa utaratibu mzuri wa uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwani kuna utofauti Mkubwa kabla ya Sheria ya NGOs kuboreshwa .

"Ukitaka kujipima umefika wapi na kama umefanikiwa angalia tulipotoka hapo mwanzo katika masuala ya usajili na uratibu wa NGOs na sasa naona mifumo imeboreshwa sana na hasa tulipoingia katika mifumo ya kidigitali" alisema Mhe. Mariam

No comments:

Post a Comment