Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KAMATI ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhishwa na jitihada za serikali chini ya uongozi wa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 16, 2023 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq kwenye kikao cha kamati cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo kwa mwaka 2022/23.
Mhe. Toufiq amesema miongoni mwa jitihada hizo ni kuanza kulipa deni la michango ya kabla ya mwaka 1999 ambapo hadi sasa kiasi cha Sh.Trilioni 2.17 kimelipwa kati ya Sh.Trilioni 4.6.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, amesema hali ya kifedha kwenye mfuko imeendelea kuimarika kufuatia uamuzi huo wa serikali kwa kulipa michango ya wanachama wa uliokuwa Mfuko wa PSPF kabla ya mwaka 1999.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Riziki Lulida pamoja na Mjumbe wa kamati, Mhe. Neema Mwandabila, wamepongeza mfuko kwa matumizi ya Tehama kwenye utoaji huduma kwa wanachama huku wakishauri iendelee kujiimarisha kidigitali ili kusomana na mifumo mingine.
Akijibu hoja za wajumbe, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, amesema uhai wa mfuko ni endelevu kwa mujibu wa tathmini iliyofanyikia mwaka 2020 na unatarajiwa kufanyiwa tathmini nyingine mwaka huu.
No comments:
Post a Comment