Mkutano wa pili wa kilele baina ya wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi uliofunguliwa na Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin. |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na wawekezaji kutoka kampuni nne za Urusi zenye nia ya kuwekeza nchini katika nyanja ya usindikaji mazao, nishati jadidifu na utengenezaji wa vifungashio vya glasi.
Kampuni hizo ni SEIES (usindikaji mazao na mitambo yake), Agrovent (kusindika mazao yanayoharibika haraka), Unigreen Energy (Nishati Jadidifu) na TD Glass NN Expo LLC (utengenezaji wa chupa za vioo vya kutumia mchanga na magadi).
Amekutana Julai 29, 2023 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza nao jijini St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.
Akielezea kuhusu kampuni yao, Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni ya SEIES, Bw. Yuri Korobov amesema wanasindika vyakula kwa kukausha mazao bila kuharibu viinilishe (nutrients) na vyakula hivyo vinaweza kuhifadhiwa kwa mwaka mmoja.
“Tukianzisha mradi huu tunaweza kuhifadhi matunda na vyakula vingi vilivyoko Tanzania. Tunatumia teknolojia ya kugandisha na kukausha maji yote bila kuharibu viinilishe. Mradi huu unaweza kupanuliwa katika wilaya na mikoa mingine nchini Tanzania kwani tumelenga wakulima walioungana kwenye vyama vya ushirika,” amesema.
Bw. Korobov ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Kuratibu Biashara za Taasisi za Umma nchini Urusi (Delovaya Rossiya) alisema wamepanga kuwafundisha wafanyakazi ili wawe na elimu ya uhandisi wa kusindika mazao hayo.
Delovaya Rossiya ambayo pia ni maarufu kama “Business Russia” ilianzishwa mwaka 2001, inaunganisha wafanyabiashara zaidi ya 7,000 na ina uwakilishi kwenye majimbo yote 85 ya Shirikisho la Urusi.
Kwa upande wake, Mmiliki wa Kampuni ya SEIES, Bw. Mikhail Mikhailov alisema kampuni hiyo pia inabuni ufundi na kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye teknolojia ya kukausha mazao. “Nchi zinazoongoza kwa teknolojia hii ni China na Uturuki, tunaamini Tanzania inaweza kushindana nao na kuwa mbele zaidi kwenye teknolojia hii.”
Kuhusu mitambo ya kukaushia mazao, alisema wanaweza kuunda mitambo ambayo ikifika nchini inakuwa rahisi kuunganisha (assembling) na rahisi kuijenga kwa haraka. “Mitambo yetu inaweza kusindika vyakula vya mafuta, vya mimea, matunda, mbogamboga, maziwa, samaki na nyama.
Alilitaja eneo jingine wanaloweza kuanzisha ni utenegenezaji wa friji zinazotumia nguvu ya jua badala ya umeme, na teknolojia ya kutengeneza nishati ya umeme kwa kutumia takataka. “Hili ni suluhisho mara mbili kwani tutapata umeme na kuhifadhi mazingira kwa kupunguza takataka,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya Agrovent, Bw. Sergey Pribysh alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana nia ya kuja kuwekeza Tanzania kwenye mazao yanayoharibika haraka kama vile maua na mbogamboga.
“Kampuni yetu ni miongoni mwa kampuni kubwa zinazozalisha mitambo ya kusindika maziwa na nyama zinazotokana na ndege kama vile kuku na bata. Tuko tayari kushirikiana na Watanzania na tumejipanga kutoa mafunzo ili kuandaa wataalamu watakaoendesha mitambo hiyo. Itabidi tuwapate maafisa kilimo ili wafundishwe jinsi mitambo inavyofanya kazi,” alisema.
Naye Bw. Aleksey Tatarinov wa kampuni ya Unigreen Energy alisema wana nia kuimarisha sekta ya nishati nchini kwani wana utaalamu wa kutengeneza umeme jua na paneli zake, umeme wa upepo na wa jotoardhi (geothermal).
Naye Mmiliki mwenza wa kampuni ya TD Glass NN Expo LLC, Bw. Andropov Vasilyevich alisema wana kampuni inayotengeneza chupa za vioo vya kutumia mchanga na magadi kwa hiyo wana nia ya kutengeneza ili wauze kwenye viwanda vingine.
Waziri Mkuu amewahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji kwani Serikali ya awamu ya sita imeweka msisitizo kwenye uwekezaji na maamuzi yao ni sahihi kwa sababu Tanzania ni mahali sahihi pa kuwekeza.
Amewaeleza wawekezaji hao kuwa Tanzania ina soko la uhakika kwa kuwa inazungukwa na nchi za Kenya, Uganda, Kongo, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji. “Unaweza kwenda kufanya biashara kokote.”
Amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea na mkakati wa ujenzi wa miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara na uwekezaji. “Tuna miundombinu ya reli, tuna barabara nzuri karibu maeneo yote nchini, tuna ndege, tunayo maziwa makuu matatu yanayowezesha usafirishaji wa bidhaa, pia malighafi tunazo za kutosha, kwa hiyo karibuni sana Tanzania.”
No comments:
Post a Comment