WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amekabidhi tuzo na vyeti kwa Wafanyakazi na wadau walioshiriki katika zoezi la kufanikisha mradi wa usimikaji wa huduma ya Intaneti katika Mlima Kilimanjaro.
Akikabidhi tuzo hizo, Mhe. Nnauye alisema mafanikio ya kuimarisha Mawasiliano ya Intaneti katika Mlima Kilimanjario ni kielelezo tosha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukuza matumizi ya TEHAMA na kukuza sekta hii ya Mawasiliano ambayo ni ingini ya ujenzi wa uchumi.
Alisema kufanikisha kwa mradi huo wa mawasiliano kunaenda kuongeza thamani Mlima Kilimanjaro sambamba na kuimarisha sekta ya Utalii nchini ukizingatia kuwa Idadi ya Watalii wanaotembelea nchi yetu imezidi kuongezeka.
"..Hivi sasa tumeanza kuona matukio yakifanyika katika Mlima Kilimanjaro, SIMBA sports Club jana tarehe 21/07/2023 imezindua jezi zake katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, Mpiga Kinubi maarufu Duniani, Siobhan Brady ni Mwanamuziki na Mpiga Kinubi aliyeshinda tuzo za Guinness kwa kupiga Kinubi katika Milima ya Himalaya, yupo Tanzania na anatarajia kupiga Kinubi akiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, ni matumaini yangu kuwa uwepo wa intaneti kutasaidia kutangaza tukio hilo sambamba na kuutanga mlima wetu.
Aidha aliongeza kuwa, zipo faida lukuki za uwepo wa mawasiliano ya Intaneti katika Mlima Kilimanjaro zikiwemo kukuza sekta ya utalii, kutengeneza mazingira rafiki kwa watalii kupata huduma za mawasiliano pamoja na watoa huduma za kitalii, TTCL kujipatia mapato kutoka kwa watumiaji huduma hizo, Serikali kupata mapato, sambamba na kuimarisha Ulinzi na usalama eneo la Hifadhi. Mradi pia utasaidia Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika utekelezaji wa mkakati wa kujenga Tanzania ya Kidijitali.
Awali akizungumza katika hotuba yake, Mkurugenzi Mkuuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Eng. Peter Ulanga alibainisha kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania litaendelea kuhakikisha huduma ya Intaneti inapatikana muda wote na yenye kasi kwa wateja wetu ili kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita(6) inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutangaza vivutio vya Utalii nchini.
"Tangu huduma hii izinduliwe huduma ya Intaneti katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, ambayo imenufaisha Watalii na wasio watalii, jumla ya zaidi ya watumiaji 24,837 wametumia huduma hiyo tangu tuanze mradi mwezi wa Agosti mwaka jana 2022 na tunatarajia kuwa katika kipindi cha msimu wa Watalii ambao umeanza sasa idadi ya watumiaji itaongezeka. Kuongezeka kwa watumiaji kutasaidia kuongezeka kwa mapato ya Shirika na nchi kwa ujumla". Alisema Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Eng. Ulanga.
Akifafanua zaidi juu ya mradi huo, Eng. Ulanga alibainisha ujenzi wa mradi huo ni kazi nzuri iliyofanywa na Wahandisi wazawa wa TTCL hivyo wana kila sababu ya kuwapongeza kwa kazi ya kizalendo waliyoifanya licha ya mazingira ya utekelezaji wa kazi hiyo kuwa magumu sana. Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru 'Porters' zaidi ya 200 waliofanya kazi ya kubeba vifaa vya mawasiliano na kupandisha katika maeneo ambayo ujenzi ulikuwa ukifanyika.
"...Hii inaonesha jinsi gani tumepiga hatua kama Taifa yakuwa na wataalam wa kuweza kufanya kazi hizi bila kuhitaji msaada wa wataalamu kutoka nje ya nchi. Kwa mara nyingine naomba ninawashukuru na kuwapongeza kwa weledi waliouonesha katika kukamilisha mradi huu kwa wakati." Alisisitiza, Eng. Ulanga katika hotuba yake.
Hata hivyo, ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya Intaneti kwenye vivutio vya Utalii nchini, TTCL imeanza ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano katika njia ya Machame Gate na inatarajia kukamilisha mradi huo kabla ya mwezi Septemba mwaka huu 2023. Aidha, mradi wa kupeleka Intaneti kwa njia ya Wi-Fi kwenye maeneo ya umma (Public Wi Fi), umeanza katika Vyuo Vikuu, ikiwemo ufungaji wa 'Wi-Fi' katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika College of Information and Communication Technologies (CoICT). Na vyuo vingine ambavyo viko katika hatua za awali za utekelezaji mradi.
"Katika utekelezaji wa Mkakati wa Shirika, hivi sasa tunatekeleza mradi wa FAIBA MLANGONI KWAKO ambapo tunapeleka huduma ya Intaneti kwenye makazi na ofisi. Huduma hii ni BURE, mteja ataingia gharama ya kununua Kifurushi tu ambacho gharama yake inaanzia shilingi Elfu Hamsini na Tano (55,000/-). Huduma hii itasaidia pia kupunguza gharama za bando kwa Wananchi wetu," alieleza Eng. Ulanga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano - TTCL Tanzania, Bi. Zuhura Sinare Muro akizungumza katika hafla hiyo, alisema Bodi ya Wakurugenzi inafarijika kuona matukio makubwa yameanza kuonekana mubashara kwenye Mlima Kilimanjaro, mbali na Serikali kupata mapato jambo ambalo linaendelea kuvitangaza vivutio vya taifa Kitaifa na Kimataifa.
Jumla ya Wafanyakazi 14 waliofanikisha zoezi hilo walikabidhiwa vyeti na tuzo wa wakiwemo wafanyakazi 11 wa TTCL na wafanyakazi watatu wa KINAPA, pamoja na makundi mengine yalioshiriki ufanikishaji zoezi zima.
No comments:
Post a Comment