BARAZA LA USHINDANI LAJIPANGA KUBORESHA MAZINGIRA NA KUONGEZA KASI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 6 July 2021

BARAZA LA USHINDANI LAJIPANGA KUBORESHA MAZINGIRA NA KUONGEZA KASI

Mshauri wa Sheria wa FCT, Bw. Kunda Mkenda akizungumza na vyombo vya habari kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo taasisi hiyo inashiriki ikiwa ndani ya Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mshauri wa Sheria wa FCT, Bw. Kunda Mkenda akifafanua jambo alipozungumza na vyombo vya habari kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo taasisi hiyo inashiriki ikiwa ndani ya Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mshauri wa Sheria wa FCT, Bw. Kunda Mkenda akisisitiza jambo kwenye mkutano huo na wanahabari (hawapo pichani) kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

BARAZA la Ushindani (FCT) limejipanga kuboresha mazingira na kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri kwa wateja ili kuleta ufanisi zaidi. 

Akizungumza na vyombo vya habari kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Mshauri wa Sheria wa FCT, Bw. Kunda Mkenda alisema lengo hilo la maboresho litakwenda sambamba na kuboresha mifumo inayotumika kusikiliza mashauri ikiwamo kurekodi, kufungua na kusajili mashauri kwa njia ya mtandao.

Alisema licha ya maboresho yajayo, FCT imefanikiwa kutoa uamuzi katika mashauri ya rufaa 215 kati ya 250 sawa na asilimia 86 yaliyowasilishwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, huku ikijipanga kuongeza kasi zaidi na ufanisi licha ya changamoto zinazojitokeza kwa wajumbe wa usikilizaji mashauri.

“Kuna kipindi muda wa wajumbe ulikuwa umemalizika, hivyo kukawa na mlundikano wa mashauri, lakini sasa wameteuliwa tayari na wataanza kazi hivi karibuni,” alisema Mkenda akizungumza ndani ya Banda la FCT Sabasaba. Baraza la Ushindani maarufu, Fair Competition Tribunal (FCT) ambalo mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama Kuu anayeteuliwa na Rais, ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoanzishwa na serikali kusikiliza na kuamua kesi za rufaa.

Rufaa hizo ni zile zinazotokana na uamuzi wa Tume ya Ushindani (FCC) na mamlaka za udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Huduma za Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasilano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).

Hata hivyo, Bw. Mkenda aliwaomba wananchi kutembelea banda la FCT ili wajue haki zao wanapokuwa wanapata na kutumia huduma mbalimbali zikiwamo za ununuzi na utumiaji wa nishati, mawasiliano na usafiri wa anga na ardhini.

Alisema rufaa nyingi za mashauri waliopokea yanatoka katika sekta za nishati, mawasiliano, usafiri wa anga na ardhini na rufaa zinazotokana na ushindani katika soko. “Mashauri mengi yametoka sekta ya nishati kupitia Ewura hususan suala la uchakachuaji wa mafuta ambao uliharibu hata magari na kusababisha kesi nyingi pamoja na hitilafu za umeme zilizosababisha baadhi ya nyumba na vifaa kuungua...” alisema Bw. Mkenda.

No comments:

Post a Comment