Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango (wa tatu kushoto) akizindua Tawi la 229 la NMB Buhigwe, Mkoani Kigoma. |
NA MWANDISHI WETU, KIGOMA
MTANDAO wa Matawi ya Benki ya NMB
nchini umezidi kutanuka, baada ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip
Mpango kuzindua Tawi la 229 la NMB Buhigwe, alilosema linaenda kuchachua kasi
ya ukuaji kiuchumi kwa wakazi wa Halmashauri hiyo, wakiwemo wadau wa Sekta za
Kimkakati - hususani za Kilimo na Biashara.
Uzinduzi wa Tawi la NMB Buhigwe
uliofanyika chini ya kaulimbiu ya: 'Tunajivunia Kukufikia na Kukuhudumia,'
umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, ukienda sambamba na
makabidhiano ya misaada ya vifaa vya elimu na afya vyenye thamani ya Sh.
Milioni 82 kwa shule, hospitali na zahanati za Buhigwe, zikiwemo Shule za
Sekondari Kahimba na Nyumbigwa, za Msingi Katema, Nyamiti na Zahanati ya Kasumo
zote za mkoani Kigoma.
Mchango huo ukamsukuma Dk. Mpango
kuitaja NMB kuwa ni Fahari ya Watanzania, sio tu kutokana na Gawio Rekodi la
Sh. Bilioni 45.5 ililotoa kwa Serikali mwezi uliopita, bali ushiriki wa taasisi
hiyo katika kutatua changamoto za jamii kupitia Program ya Uwekezaji kwa Jamii
(CSI), ilikotenga takribani Sh. Bilioni 6.2 kusaidia Jamii kwa mwaka huu
kutokana na faida yao ya mwaka uliopita wa 2022.
NMB Buhigwe linaifanya taasisi hiyo
kinara ya fedha kufikisha matawi 132 wakati huu inapoadhimisha miaka 25 ya
huduma na mafanikio ya kitaifa na kimataifa - hivi sasa ikiwa na wateja zaidi
ya milioni 6, mbali na matawi 97 iliyokuwa nayo wakati ikianzishwa mwaka 1997,
ikitambulika kama Benki ya Makabwela ilipokuwa na wateja 600,000 tu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,
ulioshuhudiwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Sadat Mussa, Dk. Mpango aliipongeza NMB kwa kuambatanisha tukio hilo na
ukabidhi wa vifaa tiba na elimu, sambamba na kulitengea tawi hilo Sh. Bil. 1 ya
kukopesha wateja na wadau wa mnyororo wa thamani wa Kilimo na Biashara, huku
akiwataka Wana Buhigwe kuzichangamkia.
Dk. Mpango Aliongeza kuwa tawi hilo
linaenda kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi, ikiwemo kumalizia changamoto ya
mikopo migumu kutoka kwa wakopeshaji wadogo 'kausha damu,' upotevu wa pesa,
uporaji na matumizi yasiyo ya lazima, lakini pia litavutia wawekezaji na kuwa
chachu ya ongezeko la akaunti za wateja na kukuza pato la taasisi hiyo, hivyo
kutanua Gawio la Serikali pamoja na fungu la Uwajibikaji kwa Jamii.
Licha ya kuishukuru na kuipongeza
NMB, Dk. Mpango aliitaka benki hiyo kuendelea kuongoza taasisi zingine katika
kufanikisha azma ya Serikali ya kusogeza huduma za kifedha kwa jamii kwa
kukagua ili kubaini maeneo yanayostahili kufikishiwa matawi na mawakala,
sambamba na kuwahimiza wakazi wa Buhigwe na Kigoma kwa ujumla kutumia huduma
hizo zinapowafikia na kuachana na utunzaji fedha kwenye mitungi majumbani.
"Wito wangu NMB na wengine
watakaofuata nyayo zenu kuja hapa, hakikisheni elimu ya fedha inawafikia
wananchi, wengi wao hapa hawajui maana au faida za hisa na hati fungani.
Hawajui umuhimu wa kukopa kwa malengo ndio maana wanaishia kutumia mikopo
kwenda kunywea pombe au kuposea wake wa ziada.
"BoT na Umoja wa Mabenki unaweza
kuongeza nguvu eneo hilo la elimu ya fedha," alisisitiza Dk. Mpango huku
akiitaka NMB yenyewe kuchangamkia fedha za Mfuko wa Mazingira Ili kujiongezea
nguvu ya kuimarisha mapambano ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kama
inavyofanya kupitia Sh. Bilioni 2 ilizotenga kwa ajili ya Kampeni Endelevu ya
Upandaji Miti Milioni moja kwa mwaka huu.
Aidha, aliitaka NMB kwamba licha ya
uimara na uthabiti wake kimtaji na kiuchumi, inapaswa kujiimarisha na kujiweka
kinga zaidi za kudhibiti athari za misukosuko itokanayo na kuyumba kwa Sekta ya
Fedha duniani kunatokana na mikwamo kama ya Majanga ya Covid na vita za
kimataifa, ambako aliiagiza BoT kuweka mkazo
wa kupambana na kuporomoka kwa Mabenki Ili kuyawezesha kuhimiri changamoto
hizo kama ilivyo NMB.
Mapema kabla ya Dk. Mpango, Afisa
Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema changamoto
ya upotevu wa muda wa kufuata huduma za kifedha mbali imemalizwa, kama
zitakavyomalizwa nyingine zilizokwaza ustawi wa kiuchumi wa wakazi wa Buhigwe,
ambao wametengewa kupitia tawi lao hilo Sh. Bilioni 1 za mikopo ya kipindi
kifupi inayoenda kuongeza thamani ya kilimo hasa kwa mazao ya kimkakati
yanayolimwa hapo.
"Tawi limetengewa Sh. Bilioni 1
ya mikopo ya haraka kwa ajili ya kuongeza thamani kwenye mazao ya kimkakati
yakiwemo mahindi, pamba, mpunga, kahawa, tangawizi, mihogo, chikichi na
mengineyo, pamoja na Biashara na ujasiriamali. Hizi ni sehemu ya jitihada za
Kimkakati za NMB kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla," alibainisha
Mponzi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, alivutiwa na namna Wana Buhigwe
walivyohudhuria kwa wingi, akiyaita mahudhurio hayo kama uthibitisho wa utayari
na kiu ya huduma za kifedha miongoni mwao na kwamba benki yake iko tayari ikiwa
na nguvu za kipesa kukidhi mahitaji ya Wana Kigoma aliowataka wajione kama
wamililiki wa hisa za NMB kupitia asilimia 31.8 ya Hisa za Serikali, hivyo
kuwasisitiza kuwa NMB ndio chaguo sahihi kwao.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Fedha
wa BoT, Sadat Mussa, aliipongeza NMB kwa kusambaza elimu ya fedha na huduma za
kibenki mjini na vijijini, na kwamba Sekta hiyo nchini inazidi kuimarika baada
ya mkwamo wa Covid na Vita ya Ukraine, ambako jumla ya Sh. Trilioni 29
zimetolewa na taasisi za fedha kama mikopo hadi kufikia Juni mwaka huu, huku
BoT yenyewe ikitenga Sh. Trilioni 1 kuyakopesha mabenki hayo.
No comments:
Post a Comment