KATIKA kukuza mchango wa Sekta ya
Kilimo kwa Pato la Taifa na kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa mkulima
mmoja mmoja na wadau wa mnyororo huo wa thamani, Benki ya NMB imesaini
makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Agricom, yatayowawezesha wakulima
wadogo, wa kati na wakubwa kukopeshwa Matrekta, Zana za Kilimo na Pembejeo
nyinginezo.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo
imefanyika jijini Dar es Salaam Jumanne Juni 27, ambapo NMB kupitia Afisa Mkuu
wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, imesema ushirikiano huo ni
muendelezo wa benki yake kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu
Hasaan ya kuboresha Sekta ya Kilimo iliyoajiri wafanyakazi takribani asilimia
70, na kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 30.
Alibainisha kwamba, wanajivunia
ushirikiano huo na Agricom, na kwamba wamejipanga vya kutosha kuibeba Sekta ya
Kilimo, yakiwemo mazao ya kimkakati, na kuwa tayari benki yake imeonesha kwa
vitendo dhamira yao ya kukwamua wakulima na wadau wake, kwa kuunda Idara Kamili
ya Kilimo kwenye taasisi hiyo ya fedha, pamoja na uwepo wa Idara ya Utafiti,
zote zikilenga kuunga mkono Serikali.
"Serikali umefanya jitihada
kubwa katika sekta hii, nasi tunasaini makubaliano ikiwa ni kuitikia wito huo
ambao unadhihirisha namna Kilimo kilivyo kipaumbele cha Serikali yetu Ili
kutanua WiGo wa Sekta ya Kilimo kuchangia Pato la Taifa.
"Lengo la ushirikiano huu ni
kukuza na kuleta mabadiliko ya kilimo kwa wakulima wa kada zote, kupitia
makubaliano haya wakulima watapata mikopo ya Matrekta, Zana za Kilimo na
Pembejeo - huruma ambazo zinatokewa na washirika wetu hawa wa Agricom.
"Msukumo wa yote haya ni NMB
kutambua umuhimu wa sekta hii kwa Uchumi Endelevu wa Taifa," alisema
Mponzi huku akibainisha kuwa, wakulima watakaokopa zana ama Pembejeo hizo za
Kilimo, watalazimika kuwa na asilimia 20 tu ya malipo ya awali.
Aliongeza ya kwamba NMB italipia
asilimia 80 inayobakia na mkopaji atakuwa huru kulipia marejesho ya mkopo kwa
msimu wa zao husika ama kulipa kwa mikupuo tofauti kutoka katika vyanzo
vinginevyo, huku akiwataka wadau kujitokeza kwenye matawi 229 ya benki hiyo kote
nchini, kupata huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji
wa Agricom Africa, Alex Duffar, alikiri kufurahishwa na kusainiwa kwa
makubaliano hayo baina ya NMB na taasisi yake aliyoitaja kama kinara wa mauzo
ya Zana Bora na za Kisasa za Kilimo, na kwamba ukubwa wa washirika hao, unaenda
kuinua wakulima na kusukuma mbele maendeleo ya Sekta ya Kilimo Tanzania.
Duffar alibainisha kuwa, Kampuni ya
Agricom ina masuluhisho mengi yanayokidhi mahitaji ya wadau wa mnyororo wa
thamani wa kilimo, walikobobea katika uzalishaji wa Pembejeo na zana muhimu
zinazokidhi hatua zote muhimu za kilimo, ikiweko utayarishaji wa ardhi na
umwagiliaji, upandaji, upaliliaji, utunzaji wa mazao na uhifadhi wake baada ya
mavuno.
Aliongeza kwamba ushirikiano baina
yao unaojumuisha Wateja wadogo, wa kati na wakubwa zaidi ya 7000, na NMB iliyo
na mtandao mpana wa matawi kote nchini, unalihakikishia Taifa ukuaji wa haraka
wa Sekta ya Kilimo na Uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, huku
akibainisha kwamba Agricom iliyoanzishwa mwaka 2009, inao wauzaji
walioidhinishwa zaidi ya 40 na matawi yapatayo 13 - wote wako wa tayari
kuhudumia wateja wa NMB watakaohitaji mikopo.
"Tunajivunia mashirikiano haya
baina ya taasisi vinara, Sisi tukiwa na mtandao mkubwa wa Wateja na matawi
mengi, kama ilivyo kwa NMB ambayo imesambaza matawi kote nchini. Ni ushirikiano
unaolihakikishia Taifa tija, kama tulivyothibitisha kupitia bidhaa zetu kwa
wakulima wa mazao ya mpunga, pamba, tumbaku, kahawa na mengineyo.
"Ushirikiano wetu huu na NMB ni
muendelezo tu, tumefanya mengi pamoja na tunaamini makubaliano haya Sasa
yanaenda kunufaisha Wateja wa pande zote mbili, kwani tunaamini katika ubora wa
bidhaa zetu na telnolojia iliyotumika katika utayarishaji wake," alisema
Duffar.
Awali, Mkuu wa Idara ya Kilimo
Biashara (Agri - Business) wa NMB, Nsolo Mlozi, alisema benki yake imefanya
uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Kilimo, ilikotoa mikopo ya mabilioni kwa
wadau, lengo likiwa ni kusapoti ustawi wa sekta hiyo nchini, huku akiwataka
wakulima kuchangamkia mikopo hiyo ya Matrekta, Zana na Pembejeo za Kilimo,
kwani Kilimo kinakosa tija iwapo kitafanywa bila zana na pembejeo bora na za
kisasa.
No comments:
Post a Comment