Na Dotto Mwaibale, Singida
WATU sita wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida wakituhumiwa
kujihusisha na vitendo vya mauaji ya watu, kufukua makaburi wilayani Manyoni na
kuchukua sehemu za siri za miwili ya watu waliozikwa kwa ajili ya kutengeneza
dawa ya kupata utajiri kuwauzia wateja wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, katika taarifa yake
Jana kwa vyombo habari, alisema watuhumiwa hao ambao hakuwataja majina kwa kuwa
uchunguzi bado unaendelea, walikamatwa kufuatia msako uliofanywa na jeshi hilo
kuanzia Machi 16 hadi 24 mwaka huu katika maeneo mbalimbali wilayani Manyoni na
vijiji jirani vya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na kuhojiwa walikiri kuhusika na
mauaji ya mtu mmoja mwanaume ambaye hajafahamika jina lake mwenye umri kati ya
miaka 40 na 45 yaliyotokea Machi 3 mwaka huu eneo la relini Manyoni huku kifo
chake ikisadikiwa kilitokana na kukanyagwa na treni kichwani na mguu wa
kushoto.
Kamanda Mutabihirwa alisema baadhi ya viungo vya mtu huyo vilikuwa pembeni
ya kiwiliwili katika njia ya treni huku viungo vya sehemu y Siri vikiwa
vimenyofolewa.
"Tulivyowahoji watuhumiwa walikiri kuhusika na tukio hilo na kueleza
kwamba walikata sehemu za siri kama nywele,kuchapa na ulimi kwa lengo la
kutengeneza dawa ili kuwapatia wateja wao wanaohitaji utajiri," alisema.
Aliongeza kuwa watuhumiwa hao pia wamekiri kujihusisha na vitendo vya
kufukua makaburi wilayani Manyoni na kuua watu kwa lengo la kupata sehemu za
viungo vya binadamu kwa ajili ya kutengeneza dawa ya kupata utajiri.
"Katika kukamilisha upelelezi wetu Jeshi la Polisi lilifanya upekuzi
katika nyumba ya mtuhumiwa mmoja wao na kufanikiwa kukuta suruali moja nyeusi
ya marehemu aliyeuawa Machi 3, 2023,vibuyu viwili vyenye shanga, kibuyu kimoja
chenye ngozi ya kondoo," alisema.
Kamanda Mutabihirwa alisema vitu vingine vilivyokamatwa kwa mtuhumiwa huyo
ni pembe ya kondoo yenye kioo na shanga,pembe ya ng'ombe yenye vipembe viwili
vidogo,vipande vitatu vya sanda,kaniki vipande viwili,kitambaa kimoja chekundu
na kopo la mafuta yenye mchanga wa kaburi na nywele.
Kufuatia hali hiyo,Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limetoa wito kwa
wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina na badala yake wafanye kazi
kwa bidii kupata utajiri halali.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza na wananchi wilayani Manyoni alisema kamati ya kuchunguza mauaji mfululizo ya watu yanayotokea wilayani Manyoni imefanikiwa kukamata watu wanaojihusisha na matukio hayo ambao wamekutwa na damu, viungo vya binadamu na nywele majumbani mwao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza jana na wananchi
wakati wa kuwasilisha ripoti ya kamati ya migogoro ya viwanja, alisema kamati
ya kuchunguza mauaji ya watu wilayani Manyoni ambayo bado inaendelea na kazi imeanza kuleta matunda
ambapo watu kadhaa wamekamatwa.
"Hapa Manyoni tuliunda Kamati tatu ikiwamo ya kuchunguza mauaji ya
watu Manyoni,ripoti ya awali ya mauaji imeanza kuleta matunda,kuna watu tayari
tumewakamata tumewakuta nyumbani kwao wana damu,wana viungo vya binadamu na
wana nywele na tayari wapo mikono ya sheria," alisema.
Serukamba ambaye hata hivyo hajutaja idadi ya watu waliokamatwa wakihusika
na mauaji hayo,alisema waliokamatwa wamemtaja mganga mmoja wa kienyeji kwamba
ndiye alikuwa anawatuma.
Mkuu wa Mkoa wa Singida aliunda Kamati ya Kuchunguza Mauaji ya watu Manyoni
hiyo Januari 21, mwaka huu wakati akisikiliza kero ambapo wananchi walipaza sauti kumuomba
aingilie kati jambo hilo.
Katika hali ya kushangaza,wananchi hao walimweleza kuwa mauji ya watu ambayo yameibua hofu kubwa kwa jamii baadhi ya pikipiki zinazomilikiwa na baadhi ya watumishi kwa ajili kuendesha biashara zao ndizo zinatumika kwenye mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment