KIWANDA CHA SINGIDA FRESH OIL MILL CHAMTWISHA CHONGOLO KERO ZA USHURU WA HALMASHAURI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 4 March 2023

KIWANDA CHA SINGIDA FRESH OIL MILL CHAMTWISHA CHONGOLO KERO ZA USHURU WA HALMASHAURI

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kukamua mafuta ya kula ya Alizeti cha Singida Fresh Oil Mill, Khalid Ally Omari (Shullu) akimuelekeza jambo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo wakati alipotembelea kiwanda hicho leo Machi 4, 2023 katika siku ya mwisho ya ziara yake mkoani hapa.Kulia ni Afisa Rasilimali watu (HR) wa kiwanda hicho, Hussein Buhuba na kulia kwa Chongolo ni  Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa,Sophia Mjema. 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

KIWANDA cha kukamua mafuta ya kula ya alizeti cha Singida Fresh Oil Mill, kimemuomba Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo,kusaidia kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazozoletesha uzalishaji ikiwamo kuwepo kwa vizuizi vingi katika usafirishaji wa bidhaa za mazao ya kilimo vinavyowekwa na halmashauri.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Khalid Ally Omary almaarufu Shulu ametoa ombi hilo Leo Machi 4, 2023 baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Chongolo alipotembelea kiwanda hicho kuangalia uzalishaji ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake mkoani hapa.

Omary alimweeza Katibu Mkuu wa CCM kuwa changamoto ambazo zimekuwa kero katika uendeshaji wa kazi ni kuwepo kwa vizuizi vingi wakati wa usafirishaji wa bidhaa za mazao ya kilimo katika barabara kuu.

 "Ukisafirisha mashudu ya alizeti kutoka Singida kwenda Kenya utapitia Singida,Oldonyosambu na Longido unatozwa ushuru kila eneo kwa bidhaa hiyo wakati jirani zetu Uganda hawana tozo yeyote ya bidhaa hiyo wakipeleka Kenya, hali hii inasababisha ugumu kushindana na waganda ambao tunategemea soko moja Kenya," alisema Omary.

Ally alitaja changamoto nyingine kuwa ni kukatikatika kwa umeme kila mara na kusababisha uharibigu wa mashine, ubovu wa barabara na uhaba wa alizeti ya kutosha.

Mkurugenzi huyo alisema kwa Sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kukamua Tani 90 kwa siku za alizeti na kupata lita 23,300 za alizeti lakini kutokana na ukosefu wa alizeti ya kutosha kinakamua tani 22 tu na kupata mafuta kita 6,600 kwa siku. 

Naye Chongolo akizungumza baada ya kukitembelea kiwanda hicho Chongolo alisema  halmashauri ziache tabia ya kuvizia kila kinachopita kwao wakichukue kwani jambo hilo linaweza kusababisha maeneo mengine yashindwe kupelekewa bidhaa.

"Hebu fikiria mtu atoke na samaki wake mjini Mwanza afike Misungwi achajiwe,apite Kishapu achajiwe,aje Shinyanga achajiwe,aje Nzega achajiwe,aje Igunga achajiwe,apite Iramba,Mkalama na Singida achajiwe,afike Ikungi hadi Manyoni achajiwe, Sasa je bidhaa hiyo hadi ifikishwe Dar es Salaam itauzwa kwa shilingi ngapi," alisema.

Chongolo alisema hali hiyo inakuwa hivyo kwasababu kila halmashauri inashindwa kubuni mfumo na uwekezaji wa kwao na hivyo kutaka kuibukia na kutengeneza sheria ndogo zenye lengo la kuwaumiza wengine jambo ambalo CCM haikubariani nalo.

Alisema ni lazima mamlaka zinazohusika ziweke mifumo na sheria ndogo ambazo zitakwenda kusimamia ukusanyaji wa mapato katika halmashauri na kwamba sheria hiyo ziwekwe wazi kwenye mazao yanayozalishwa katika eneo husika ili kudhibiti kudai ushuru katika kila eneo mazao yanapopita.

Chongolo kabla ya kutembelea kiwada hicho  alifungua mradi wa kiuchumi wa fremu za maduka katika eneo la Ofisi za CCM mkoa Singida mjinina vile vilivyopo Uwanja wa Namfua.

 Mkurugenzi wa Kiwanda cha kukamua mafuta ya kula ya Alizeti cha Singida Fresh Oil Mill, Khalid Ally Omari (kushoto) akimpatia boksi lenye mafuta ya kula Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo wakati alipotembelea kiwanda hicho leo Machi 4, 2023 katika siku ya mwisho ya ziara yake mkoani hapa.Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata na kutokakushoto ni Katibu wa CCM  Mkoa wa Singida, Lucy Boniface na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.


Msimamizi wa kiwanda hicho, Jamari Juma akisoma taarifa ya kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha kukamua mafuta ya kula ya Alizeti cha Singida Fresh Oil Mill, Khalid Ally Omari (wa pili kushoto) akimuongoza Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kutembelea kiwanda hicho.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha kukamua mafuta ya kula ya Alizeti cha Singida Fresh Oil Mill, Khalid Ally Omari (Shullu) akimuelekeza jambo Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongo wakati wa ziara hiyo.

Msimamizi wa kiwanda hicho, Jamari Juma (katikati) akielekeza jambo wakati wa ziara hiyo.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, akipitia taarifa ya kiwanda hicho.

Muonekano wa kiwanda hicho.
 

No comments:

Post a Comment