BRT III KUKAMILIKA MACHI MWAKANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 27 February 2023

BRT III KUKAMILIKA MACHI MWAKANI

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja Mradi wa BRT, Eng. Barakaeli Mmari alipokagua maendeleo ya Ujenzi wa BRT III inayoanzia Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Meneja Mradi wa BRT, Eng. Barakaeli Mmari akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa BRTIII kuanzia Posta ya Zamani hadi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Meneja Mradi wa BRT, Eng. Barakaeli Mmari akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa BRTIII kuanzia Posta ya Zamani hadi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Msimamizi wa Ujenzi wa Barabara ya BRT III inayoanzia Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto, Eng. Hendrishi Nyange akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya mradi huo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia) na Meneja wa BRT Eng. Barakaeli Mmari (kushoto), wakikagua makalvat yatakayotumika katika ujenzi wa Mradi wa BRT III unaoendelea jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa wataalam wa  Wakala wa Barabara nchini, TANROADS alipokagua maendeleo ya Ujenzi wa BRT III unaoanzia Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Moja ya mtambo unaotengeneza barabara za BRT III ukiandaliwa na mafundi kabla ya kuanza kazi hiyo.

Muonekano wa Barabara ya BRT III ambayo ujenzi wake kiwango cha zege unaendelea jijini Dar es salaam.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa Barabara ya Mabasi yaendayo haraka – (BRT) III na kumtaka mkandarasi Sinohydro anaejenga Barabara hiyo kuhakikisha inakamilika ifikapo Machi Mwakani.

Akizungumza alipokagua ujenzi huo Prof. Mbarawa amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanaotumia Barabara hiyo inayoanzia Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho ujenzi huo unaendelea.

“Nia ya Serikali ni kupunguza msongamano jijini Dar es Salaam hususan barabara hii inayokwenda katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julias Nyerere hivyo hakikisheni ujenzi unakwenda kwa haraka na ubora ili kuleta tija kwa Wananchi,” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha amewataka madereva wa magari katika barabara ambazo ujenzi wake bado unaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakandarasi ili kulinda usalama wa abiria, wajenzi na magari kwa ujumla.

“…TANROADS hakikisheni magari yanaongozwa vizuri wakati wa asubuhi na jioni katika kipindi hiki ujenzi ukiendelea kwani hatuhitaji ajali zitokee hivyo tutii maelekezo ya wataalam wetu yenye nia ya kupunguza msongamano na kulinda usalama wa watu na magari,” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Waziri huyo wa ujenzi ameitaka TANROADS kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi waliojirani na mradi huo na kuwataka watakaopata kazi kuwa wazalendo kwa kuepuka  vitendo vya hujuma na wizi.

Naye Meneja wa Mradi wa BRT , Eng. Barakaeli Mmari amesema mradi huo wenye kilometa 23.3 utakuwa na vituo vidogo 32, vituo vikubwa 2 na daraja moja la waenda kwa miguu utakapokamilika na kupunguza msongamano.

Aidha amesisitiza kuwa TANROADS imejipanga vizuri kumsimamia mkandarasi ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati, ubora na kuleta tija kwa wananchi na taifa.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam Eng. Harun Senkuku amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaendana na program ya kupendezesha jiji kwa kuweka miundombinu rafiki kwa watumiaji wa barabara na yenye mvuto ili kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Zaidi ya Shilingi bilioni 231.7 zinatarajiwa kutumika katika mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Machi Mwakani na hivyo kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji la Dar es Salaam na barabara ya Nyerere.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasilino Serikalini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

No comments:

Post a Comment