BIMA YA AFYA KWA WOTE,UBORA WA HUDUMA KUIMARISHWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 19 January 2023

BIMA YA AFYA KWA WOTE,UBORA WA HUDUMA KUIMARISHWA


Na Faustine Gimu, Kilimanjaro

MKURUGENZI wa Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Dkt. Leonard Subi amesema kuanzishwa kwa Bima ya Afya kwa Wote  kigezo cha ubora wa Huduma kitaangaliwa katika vituo vyote vya kutolea huduma ili kuhakikisha kila Mwananchi anakuwa na fursa ya kupata matibabu kwa ufanisi.

Dkt. Subi amebainisha hayo Mkoani Kilimanjaro wakati akitoa mafunzo kwa watalaam wa Afya ya Uzazi na Mtoto kanda ya Kaskazini katika kikao kilicholenga kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

Dkt. Subi amesema Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote patakuwa na uhimilivu na ustahimilivu wa mifuko hivyo ni jambo la msingi kwa wananchi kuendelea kuelimishwa 

“Inawezekana wapo watu kule wanakosa huduma au wanashindwa kuzifikia huduma kwa sababu hawana Bima ya Afya, kwa hiyo Bima ya Afya kwa Wote itakuwa mkombozi wetu, kutakuwa na uboreshaji mkubwa huduma za afya kama mnavyofahamu serikali yetu imejenga Hospitali hata zile wilaya ambazo hazikuwa na hospitali,” amesema Dkt. Subi.

Dkt. Subi ameendelea kufafanua kuwa serikali imejipanga katika bajeti ya dawa kwenye Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote huku vitita vya mafao vikiendelea kuboreshwa siku hadi siku pindi Muswada utakapopitishwa kama sheria hivyo ni muhimu kila mwananchi kujiandaa ili aweze kupata fursa hii muhimu.

Kuhusu suala la utoaji huduma kwa lugha yenye staha kwa watumishi kada ya Afya ,Dkt.Subi amesema serikali itaendelea kulisimamia ili kuhakikisha kila mhudumu anakuwa  na lugha nzuri kwa mteja.

“Kuhusu suala la Customer Care, lazima malalamiko yapungue, kwenye Bima ya Afya kwa Wote  hakuna mtumishi atakayekuwa na lugha chafu,” amesema.

Aidha, Dkt. Subi ametaja faida zingine zitokanazo na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote ni kuimarisha uchumi wa kila mwananchi kwani fedha alizokuwa anatarajia kwenye mambo ya matibabu atazitumia kwenye mambo mengine ya maendeleo.

“Kumbukeni gharama za matibabu zimekuwa kubwa kama hauna bima ,sasa hivi ukienda tu CT-Scan  150,000 hadi 200,000 ,mtanzania wa kawaida ataitoa wapi, lakini akiwa na Bima maisha ni kuteleza tu,kupasuliwa ubongo milioni, ukiwa na bima unapasuliwa unarudi nyumbani hivyo Bima ya Afya kwa wote itaimarisha mapato ya Mtanzania,’’amesema.

Mganga Mfawidhi  Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi Dkt. Edna Munisi amesema Bima ya Afya kwa Wote itasimamia haki ya kila mtu na serikali kuwagharamia wasiokuwa na uwezo.

Ikumbukwe kuwa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajia kusomwa Bungeni mwishoni mwa mwezi huu na endapo utapitishwa kama sheria utaanza kufanya kazi rasmi mwezi Julai, 2023.

No comments:

Post a Comment