TAARIFAYA UTEKELEZAJI MAJUKUMU NA MAFANIKIO YA TMA KWA MWAKA 20021/22 - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 2 November 2022

TAARIFAYA UTEKELEZAJI MAJUKUMU NA MAFANIKIO YA TMA KWA MWAKA 20021/22

 TAARIFAYA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU NA MAFANIKIO YA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA KWA MWAKA WA FEDHA 20021/22 NA MWELEKEO WA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2022/23, UKUMBI WA IDARA YA HABARI-MAELEZO, PSSSF, DODOMA.


Ndugu wanahabari;Nianze kwa kuwasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Awali ya yote napendakumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetuwezesha kukutana hapa leo tukiwa na afya njema. Pia, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa utayari wenu wa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kila tunapowahitaji katika jukumu la kuwafikishia wananchi na wadau taarifa muhimu zinazohusu masuala ya hali ya hewa, kwani mmekuwa daraja kwetu na jamii. Napenda kuchukua fursa hii tena kuwashukuru sanakwa mchango wenu mkubwa kwa ustawi wa Taifa letu.

Dhumuni la mkutano wetu huu leo hii ni kutoa taarifa ya Utekelezaji wa majukumu na mafananikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Pia nitaainisha mikakati ya kuboresha huduma za Hali ya Hewa Nchini.

Ndugu Wanahabari, kwanza nianze na historia fupi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019 kupitia Tangazo la Serikali GN.459 la tarehe 14 Juni, 2019 ikiwa na jukumu la kuratibu, kudhibiti na kutoa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mamlaka hii imetokana na iliokuwa Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania ilioanzishwa kwa Sheria ya Wakala (Executive Agencies Act) Sura Na. 245 marejeo ya mwaka 2002. Kabla ya Wakala wa Hali ya Hewa, huduma za hali ya hewa nchini zilikuwa zinatolewa na iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa nchini (Directorate of Meteorology) ambayo ilianzishwa Mwaka 1978 baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ikiwa na jukumu la kufanya uangazi na kutoa taarifa za hali ya hewa nchini. Kabla ya Jumuiya ya Afrika Mashariki huduma za hali ya hewa nchini zilitolewa chini ya Taasisi ya Hali ya Hewa iliyokuwa chini ya wakoloni.

Ndugu Wanahabari, naomba sasa mniruhusu nizungumzie Utekelezaji wa Majukumu ya TMA. Majukumu ya Mamlaka yamegawanyika katika sehemu kuu tatu; sehemu ya kwanza ni kutoa huduma za hali ya hewa; sehemu ya pili ni kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha kumi na nne (14) na sehemu ya tatu ni kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini Tanzania kulingana na Kifungu cha tano (5) cha Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019. 

Aidha, Mamlaka ina jukumu la kuiwakilisha nchi katika masuala ya kiufundi (technical matters) ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa.

Pamoja na utelezaji huo kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019, vilevile, Mamlaka imekuwa ikifuata miongozi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SGDs), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano iii 2021/22-2025/26, Ilani ya Chama cha Mapinduzi 200-2025 na Mpango Mkakati wa TMA.

Ndugu Wanahabari, Katika utelekezaji wa majukumu yake katika mwaka wa fedha 2021/22 Mamlaka ya Hali ya Hewa imepata mafanikio mengi. Baadhi ya mafanikio hayo ni kama ifuatavyo

1. Katika mwaka wa fedha 2021/22, Mamlaka iliendelea na utekelezaji wa mradi wa Rada, Vifaa na miundombinu ya hali ya hewa ambapo hatua mbalimbali zilifikiwa. Hatua hizi ni pamoja na kukamilika kwa asilimia 90 ya utengenezaji wa mtambo wa rada mbili (2) za Mbeya na Kigoma ambapo pia malipo ya asilimia 90 yalifanyika. 

Mafunzo kwa wahandisi na waendesha mitambo kuhusu kuzihudumia na kuzitumia Rada hizo yalifanyika kiwandani nchini Marekani; ujenzi wa miundombinu ya Rada za Mbeya na Kigoma umekamilika; utengenezaji wa Rada mbili (2) za mwisho zitakazofungwa KIA na Dodoma ulifikia asilimia 45 ambapo Mamlaka ilifungua barua ya dhamana kwa ajili ya malipo ya asilimia 80 ya utengenezaji wa Rada hizo. Kukamilika kwa Rada hizi kutakamilisha mtandao wa Rada nchini kwa idadi ya Rada saba.Rada hizi zinauwezo wa kuona zaidi ya kilometa za mkato 450 huku zikizunguka na kuona matone madogo sana ya mvua katika hali ya uhalisia ndani ya kilometa 250. Aidha, mitambo hii pia inasaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisi wa anga letu la Tanzania.

2. Utekelezaji mwingine ni kufungwa kwa Mitambo miwili (2) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika na “measuring cylinders” zipatazo 100; Seti tano (5) za vifaa vya kutambua matukio ya radi; Vifaa 15 vya kupima mgandamizo wa hali ya hewa; vifaa 25 vya kupima kiasi cha joto na unyevunyevu; mitambo minne (4) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe; vifaa vya kupima mvua vinavyojiendesha vyenyewe. Aidha, Mamlaka imepokea kompyuta maalum “Cluster Computer” ambayo ipo katika hatua ya ufungaji; Vilevile Mamlaka ilizinduwa mfumo mpya wa uangazi wa hali ya hewa ya anga ya juu katika kituo cha kupima hali ya hewa ya anga ya juu kilichopo JNIA. 

Mamlaka iliingia mkataba wa ununuzi wa vifaa na mitambo mbalimbali ya hali ya hewa ikiwemo mitambo nane (8) ya kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga; mitambo 13 ya kupima hali ya hewa mahususi kwa sekta ya kilimo. Aidha, Mamlaka ilifungua hati ya dhamana (Letter of Credit) ya asilimia 80 kwa ajili ya mitambo hiyo;

3. Mamlaka imeendelea kutekeleza jukumu la kutoa utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku 5, siku 10, msimu na tahadhari ambapo usahihi wa utabiri katika kipindi husika ulikuwa asilimia 93.8 ukiwa juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika kimataifa;

4. Huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga ziliendelea kutolewa kwa kuzingatia mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma (ISO 9000:2015) ambapo jumla ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika mwaka 2021/22 ukilinganisha na ndege 35,111 zilizohudumiwa katika mwaka 2020/21 ambalo ni ongezeko la asilimia 13. Ongezeko hili linatokana jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na serikali yetu pamoja kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuhakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa;

5. Mamlaka imeendelea na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu kupitia ofisi zake zilizopo kwenye Bandari za Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika. Huduma hizi zimechangia kuongezeka kwa usalama na ufanisi wa shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye maji ikiwemo usafiri, shughuli za bandari, uvunaji wa gesi asilia n.k. Katika mwaka 2021/22, idadi ya watumiaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya maji iliongezeka na kufikia 36,774 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na watumiaji 32,736 waliohudumiwa katika mwaka 2020/21. Kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za hali ya hewa kumetokana na utekelezaji wa Sheria Na. 2 ya mwaka 2019 ambapo lengo ni kuboresha huduma na pia utoaji wa elimu kwa umma juu ya kutumia taarifa za hali ya hewa;

6. Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki, jukumu lingine la kimataifa nikusaidia ufuatiliaji wa ubora na upatikanaji wa data za hali ya hewa kwa vituo vya hali ya hewa vilivyo katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Sudan ya Kusini kupitia kituo cha Kanda kilichopo Tanzania. Matukio mbalimbali ya kutopatikana kwa data yaliripotiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa ajili ya kupata msaada zaidi na pia kiliendelea kutoa ripoti za kila mwezi ambazo zilitumwa kwa nchi za Afrika Mashariki;

7. Mamlaka ilipata hati safi ya ukaguzi wa hesabu katika ukaguzi wa mwaka 2020/21 uliofanywa na wakaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Uboreshaji kwenye mifumo ya kihasibu ulifanyika ambapo Mamlaka ilihamia katika Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE). Aidha, katika ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ilipata alama ya asilimia 88 ambayo inaonyesha kuwa Mamlaka inazingatia matakwa ya Sheria katika utekelezaji wa shughuli za manunuzi.

8. Mamlaka imeendelea na juhudi za kuongeza mapato kwa kuwafikia wadau mbalimbali na kuwaeleza juu ya umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa na pia kuchangia huduma za hali ya hewa kama ilivyoelekezwa katika Sheria Na. 2 ya mwaka 2019. Jitihada hizo zimepelekea mapato ya Mamlaka kuongezeka kwa asilimia 53% katika mwaka wa fedha 2021/22. 

9. Mamlaka imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza gharama za uendeshaji wa Taasisi ambapo imeweka mkazo katika kutumia TEHAMA kwa ajili ya uendeshaji na utoaji wa huduma. Mifumo ya TEHAMA iliyobuniwa na wataalam wa Mamlaka ni pamoja na DMO, MAIS, MMIS, TMA Data Exchange kwa ajili ya shughuli za uangazi, mawasiliano ya data za hali ya hewa na pia kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa usafiri wa anga na maji. Mifumo ya TEHAMA pia imeiwezesha kutoa huduma mahsusi kwa sekta za madini, usafiri wa barabara, ujenzi na utalii;

Ndugu wanahabari,Katika kuangalia ustawi wa wafanyakazi, watumishi wa Mamlaka wameendelea kuboreshewa maslahi yao kupitia kupandishwa vyeo, kubadilishwa Kada na kuhuishwa kwa miundo  ya kada kwa watumishi wa Mamlaka kufuatia Mabadiliko ya Miundo ya Maendeleo ya watumishi (Schemes of Services). 

10. Aidha,TMA imeendelea na utekelezaji wa mpango wa mafunzo kwa watumishi ambapo jumla ya wafanyakazi 50 walikuwa masomoni katika ngazi za (PhD, MSc, BSc and Diplomas) ndani na nje ya nchi, kati yao 3 PhD; 11 MSc.; 34 BSc.; 1 BA; na 2 ngazi ya shahada;

11. Katika Utendaji wake Mamlaka ilitekeleza azma ya Serikali kwa kuhamishia Ofisi za Makao Makuu Dodoma ambapo kwa sasa Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania zipo katika Jengo la Chuo Kikuu cha Dodoma. Jitihada za kujenga jengo la Makao Makuu zinaendelea kufanyika ambapo tayari kiwanja kimeshapatikana.

12. Kukamilika kwa ukarabati wa majengo ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (National Meteorological Training Centre - NMTC) kilichopo mkoani Kigoma; Mamlaka imeendelea na ukarabati wa vituo vya hali ya hewa ambapo jumla ya vituo nane (8) vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, Dodoma, Tabora, Mpanda, Mahenge, Songea na Shinyanga vilikarabatiwa;

Ndugu wanahabari na Watanzani wote kwa ujumla,katika utekelezaji wa mwaka wa fedha wa 2022/23, Mamlaka ya Hali ya Hewa imepanga mikakati kadhaa itakayosaidia katika utoaji wa huduma za Hali ya Hewa Nchini. Baadhi ya Mikakati hiyo ni kama ifuatavyo 

i) Kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa huduma za hali ya hewa;

ii) Kuendelea na utekelezaji wa Sheria Na.2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake; 

iii) Kuimarisha uangazi wa hali ya hewa katika Bahari na Maziwa Makuu ili kuimarisha usalama wa abiria wa kwenye maji, shughuli za uvuvi pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali zikiwemo upakuaji wa mizigo bandarini na uvunaji wa gesi asilia;

iv) Kufanya ufuatiliaji kwa wakandarasi wanaotengeneza Rada na vifaa vya hali ya hewa ili vikamilike na kuwasili nchini;

v) Kuongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa;

vi) Kuhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake;

vii) Kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa

viii) Kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

Kwa kumalizia, Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Idara ya Habari-MAELEZO  kwa kuratibu mikutano hii, kwa kipekee nimshukuru Rais wetu mpendwa, Mhe.Samia Suluhu Hassan,Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya kwa kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa hapa nchini ikiwemo kutenga fedha katika bajeti ya Maendeleo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Sekta ya hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa vifaa hali ya hewa, upanuzi wa mtandao wa vituo vya hali ya hewa, ukarabati wa vituo vya hali ya hewa pamoja na ununuzi wa mitambo ya hali ya hewa ikiwemo Rada.

Aidha, niendelee kuwaomba kwa kuwasisitiza kuboresha ushirikiano baina yetu hususan katika kuhabarisha umma kuhusu hali ya hewa ya kila siku, msimu na tahadhari, nazungumza hayo kwa kuwa Mamlaka imeandaa utaratibu mzuri wa kuwatumia taarifa hizo kila siku kupitia njia mbalimbali, mpaka hivi sasa vyombo vya habari tisini viko katika utaratibu huo, natoa rai kwa wengine pia kuleta maombi ya kupata huduma hii muhimu kwa jamii na nchi kwa ujumla.

Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza, 

Karibu kwa maswali.

No comments:

Post a Comment