MATOKEO YA SENSA YA WANYAMAPORI TANZANIA, NYATI WAONGOZA...! - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 1 November 2022

MATOKEO YA SENSA YA WANYAMAPORI TANZANIA, NYATI WAONGOZA...!

 

Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi Dkt. Pindi Chana akikata utepe ya ripoti ya matokeo ya sensa ya wanyamapori mara baada ya kutangaza matokeo hayo leo Jijini Arusha ambapo katika matokeo hayo Tanzania imeongoza kuwa na nyati wengi barani Afrika.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ametangaza matokeo ya sensa ya wanyamapori iliyofanyika mwaka huu ambapo Tanzania inatajwa kuongoza kwa idadi  kubwa ya nyati Barani Barani Afrika kwa kuwa na jumla ya nyati 191,805.

Akitangaza matokeo hayo Novemba Mosi, 2022 Jijini Arusha, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amesema nyati hao wengi wanapatikana katika mifumo ikolojia ya Serengeti (69,075)  Nyerere-Selous-Mikumi (66,546) Katavi-Rukwa (35,273) pamoja na Ruaha-Rungwa (20,911).

Amesema lengo la Sensa hiyo ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitatu katika mfumo Ikolojia wa Katavi – Rukwa na Ruaha-Rungwa ni kujua uwepo, idadi, mtawanyiko pamoja na viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori nchini Tanzania.

Akizungumzia kuhusu idadi hiyo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema imeendelea kuongezeka hasa katika maeneo ya ndani ya hifadhi ambapo nyati hao wameongezeko kwa asilimia 64 toka mwaka 2018.

 Amefafanua kuwa licha ya  kuwepo kwa changamoto za mifugo katika mifumo ya  Ikolojia nyati wameongezeka na hii ni kiashiria kizuri cha udhibiti wa mifugo kwenye maeneo yaliohifadhiwa.

Akizungumzia matokeo ya sensa katika mfumo wa ikolojia wa Katavi Rukwa, Waziri Dkt. Pindi Chana amesema idadi ya tembo imeendelea kuimarika na viashiria vya ujangili wa tembo vimeendelea kupungua ukilinganisha na sensa ya mwaka 2018.

Amefafanua kuwa mamo mwaka 2021, uwiano wa mizoga mipya ya tembo ilikuwa asilimia 3 wakati mwaka 2018 ilikuwa asilimia 12.

Katika hatua nyingine, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema katika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha- Rungwa idadi ya wanyamapori adimu kama korongo na palahala imeendelea kuongezeka. Korongo wameongezeka mara mbili toka korongo 1,436 mwaka 2018 hadi 3,127 kwa sensa ya mwaka 2021.

Zoezi hili liliwezeshwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori (Wildlife Conservation Society - WCS) na kuratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania.

No comments:

Post a Comment