Na Mohamed Saif
KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni Tisa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji Wilayani Makete Mkoani Njombe.
Ameyasema hayo wilayani humo Oktoba 13, 2022 wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Maji wa Mbalache- Lupombwe.
Mhandisi Sanga amesema Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020-2025 imeielekeza Wizara ya Maji kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 huduma ya maji iwe imewafikia wananchi wengi zaidi.
“Rais wetu mpendwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza ifikapo Mwaka 2025 iwe jua iwe mvua lazima huduma ya maji maeneo yote vijiji ifike asilimia 85 ama zaidi ya hapo na asilimia 95 ama zaidi kwa maeneo yote ya mijini,” amesema Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga amefafanua kuwa mradi huo wa shilingi bilioni 1.2 wa Mbalache –Lupombwe, unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali, Wahisani kutoka Jumuiya ya Kanisa la Kilutheri ya Hamburg Blankenese Ujerumani kupitia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kusini Kati (Makete) kupitia Jimbo la Mashariki Lupila, Usharika wa Lupombwe.
“Serikali kupitia Wizara ya Maji tunatoa shukrani za dhati kabisa kwenu nyinyi kama Taasisi ya Dini lakini pia kwa wenzetu, marafiki zetu kutoka Hamburg kwa msaada huu mkubwa walioutoa kwa wananchi wetu hawa, tunasema asanteni sana,” amesema Mhandisi Sanga.
Alisema Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana na Taasisi za Dini katika kuwapatia huduma bora ya maji wananchi wake na kwamba pale ambapo Taasisi ya Dini itajenga mradi wa maji Wizara itashiriki kikamilifu.
Akizungumzia hali ya huduma ya Maji wilayani humo, Mhandisi Sanga amesema Wizara inahakikisha inajenga miradi mingi kadri itakavyowezekana na pia inaboresjha miradi iliyopo ili kuwasogezea wananchi huduma ya maji.
“Tunaipitia miradi ya Ludilu-Kijombo, Maranduku na Ukange ili kuiongezea ubora zaidi na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya maji ili tuweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na mwezi ujao tutatoa shilingi milioni 400 ili kuboresha miradi hii,” amesema Mhandisi Sanga.
Vilevile amebainisha kuwa kwa mwaka huu wa fedha Wizara itaendelea kutoa fedha za kujenga miradi ya Ujuni-Nkenja, Magoye, Lupalilo na Tandala, Ipelele na Ipepo, Luwumbu, Utanziwa, Kidope Madihani, Usalimwani Mfumbi na Ruaha.
“Lakini ipo miradi inayoendelea ikiwemo ya Ikete, Uganga, Idende-Unenamwa, Lupila, Utweve Mbalache-Lupombwe hii pia tutaendelea kuitaia fedha ili iweze kukamilika na itoe huduma ya maji kwa wananchi wa wilaya hii ya Makete,” amesema Mhandisi Sanga.
Aidha alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maji inajenga zaidi ya miradi 1,000 katika maeneo mbalimbali kote nchini lengo likiwa ni kuwasogezea huduma ya majisafi na salama wananchi wake.
“Kila kona ya nchi hii kuna mradi unajengwa na niwahakikishie miradi mingi inayojengwa kipindi hiki ni miradi yenye ubora mzuri na hata kwenye Mbio za Mwenge mwaka huu miradi iliyokaguliwa ilipongezwa na viongozi wa mbio za mwenge,” amesema Mhandisi Sanga.
Aliwapongeza wataalam Wizara ya Maji kwa kuhakikisha ubora wa miradi lakini pia aliwapongeza Viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi Wilayani Makete kwa jitihada zao, ufuatiliaji na usimamizi wa ujenzi wa miradi ya maji wilayani humo.
Awali Katibu Mkuu wa KKT Dayosisi ya Kusini Kati, Mchungaji Ezekiel Sanga alisema mradi wa Mbalache- Lupombwe unajengwa kwa awamu mbili na kwamba awamu ya kwanza imekamilika na awamu ya pili inatarajiwa kukamilika ifikapo Januari 2023.
Amesema mradi utanufaisha wananchi 2,308 kutoka vijiji vya Mbalache na Lupombwe pamoja na taasisi zilizopo kwenye vijiji hivyo ambazo alizitaja kuwa ni zahanati mbili, shule ya sekondari moja, kituo cha afya kimoja, shule za msingi mbili pamoja na taasisi za dini.
No comments:
Post a Comment