Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mkakati ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo Justice Kijazi akielezea mkakati wa zao hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Wakuu wa wilaya wakiwa kwenye kikao hicho. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023/2024 inatarajia kutenga
Sh.Bilioni 4.6 kwa ajili ya kununua zana za kilimo Mkoa wa Singida.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameyasema hayo kwenye kikao cha kupanga
mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti kilicho washirikisha mkuu wa
mkoa, wakuu wa wilaya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri pamoja na maafisa
kilimo ambacho kiliketi leo Oktoba 5, 2022 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa.
Alisema Serikali baada ya kununua zana hizo halmashauri zitatakiwa zitenge
maeneo maalumu ambapo zana hizo zitawekwa na kutakuwepo mtu maalum wa
kuzisimamia na wakulima watakuwa
wakienda kukodisha.
Alisema fedha zitakazopatikana baada ya wakulima kukodi zana hizo
zitarudishwa Serikalini na kwenda kununua zana hizo katika mikoa mingine.
Awali akitoa mchanganua wa bajeti ya ununuzi wa zana hizo Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mkakati ya
kuongeza uzalishaji wa zao hilo Justice Kijazi alisema Halmashauri za Wilaya za
Ikungi,Mkalama, Iramba na Itigi kila moja zitahitaji zana zenye thamani ya
Sh.706 Milioni.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni itahitaji Sh.791Milioni huku
Singida DC ikiwa ni Sh.309 Milioni.
Akizungumzia kuhusu mpango mkakati wa zana hizo Kijazi alisema ni
kuimarisha upatikanaji wa zana bora za kilimo, mkoa unaboresha mazingira ya
uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa zana za kilimo, kuanzisha vituo vya umahiri
wa zana (Agricultural mechanization hub) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo.
Alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuwaelimisha wakulima kuhusu mikopo ya
kibenki yenye lengo la upatikanaji wa zana bora za kilimo kwa masharti nafuu na
Mfuko wa Pembejeo (AGITF) uwezeshe wakulima upatikanaji wa mikopo nafuu ya zana
za kilimo mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alisema mkoa umejipanga kusimamia
kilimo ili kiwe sababu ya kuondoa umasikini kwa wananchi.
“Mheshimiwa Waziri napenda kukuhakikishia kuwa hapa Singida kazi kubwa ni
kilimo tutakifanya usiku na mchana ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu na
maelekezo yako yote tutayafanyia kazi” alisema Serukamba.
Serukamba alisema awali watu walidhani kuwa kilimo ni jambo la kawaida na la mtu binafsi lakini sasa ni biashara na mkombozi kwa wananchi na kuwa wanazipongeza jitihada zote zinazofanywa na Serikali za kuinua kilimo na wao kama mkoa wanaziunga mkono na kutekeleza maagizo yote waliyopewa.
No comments:
Post a Comment