PROF. MBARAWA AWATAKA WAHANDISI KUIBUA NA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 22 September 2022

PROF. MBARAWA AWATAKA WAHANDISI KUIBUA NA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa,akizungumza wakati akifungua maadhimisho ya 19 ya siku ya wahandisi nchini yaliyofanyika  leo jijini Dodoma.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Aisha Amour, akisisitiza jambo kwa wahandisi (hawapo pichani), wakati wa maadhimisho ya 19 ya Siku ya Wahandisi, yaliyofanyika leo jijini Dodoma.

Wahandisi zaidi ya 200 wakila kiapo cha utii katika maadhimisho ya 19 ya Siku ya Wahandisi,yaliyofanyika leo jijini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, akizungumza katika maadhimisho ya 19 ya Siku ya Wahandisi, yaliyofanyika leo  jijini Dodoma.


SERIKALI imeahidi kuendeleza, kuibua, kutambua, kukuza na kuendeleza ubunifu unaofanywa na wahandisi wazawa kwa maendeleo endelevu ya Taifa.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema hayo leo wakati akifungua maadhimisho ya 19 ya siku ya wahandisi nchini ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria ya kuwawezesha wazawa katika ujenzi wa miradi ili kunufaika kiutalaamu, kiuzoefu na kiuchumi.


“Wahandisi ndio nguzo muwe na weledi na umakini katika kusimamia miradi ili iwe bora yenye gharama nafuu na inayokamilika kwa muda uliopangwa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.


Prof. Mbarawa ameaigiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kuchukua hatua stahiki za kisheria na za haraka kwa makampuni ya kihandisi, Taasisi na wahandisi wasio waadilifu.

 

Amesema serikali itaendelea kutekeleza miradi mingi ya kimkakati katika kujenga miundombinu na uchumi wa nchi hivyo ni jukumu la wahandisi kuitumia fursa hii muhimu kujenga Taifa lao.

Ameitaja baadhi ya miradi ambayo ujenzi wake unaendelea kuwa ni ujenzi wa reli ya SGR, Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Bandari za Dar es salaam,Tanga na Mtwara, miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara, viwanja vya ndege, maji na umeme.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewapongeza na kuwashukuru wahandisi  kwa kujenga miundombinu  mingi na ya kisasa jijini Dodoma ikiwemo reli, barabara, maji na majengo pia amewataka kuzidi kujenga uaminifu ili waweze kuaminika na kupewa kazi zaidi.

Msajili wa Bodi ya Wahandisi, Mhandisi Bernard Kavishe, akizungumza katika maadhimisho ya 19 ya Siku ya Wahandisi, yaliyofanyika leo jijini Dodoma.

Aidha, amewakaribisha kuangalia fursa za uwekezaji katika mkoa wa Dodoma ili kuuwezesha kuwa na hadhi ya makao makuu ya nchi.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Mhandisi Balozi Aisha Amour, amesema maadhimio yote yanayotolewa kwenye maadhimisho hayo yatafanyiwa kazi kwa wakati ili kuendeleza na kuleta tija katika sekta zinazohusu wahandisi nchini.

“Tumejipanga kuhakikisha kazi nzuri zinazofanywa na wahandisi zinaendelezwa na kuhakikiwa ili ziwe kwenye ubora unaokubalika wakati wote”, amesema Balozi Aisha.

Kwa upande wake Msajili wa ERB, Mhandisi Bernard Kavishe, ameeleza kuwa mpaka sasa Bodi imesajili wahandisi 33,773 ambapo kati ya hao wahandisi wanawake ni 4,012 sawa na asilimia 12.98 na kusisitiza Bodi itaendelea kuwaendeleza wahandisi wanawake.

Maadhimisho ya 19 ya Siku ya Wahandisi yanaongozwa na kauli mbiu “Ubunifu na Uendelezaji wa Ujuzi katika Kuimarisha Maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Taifa: Mtazamo wa Kihandisi”.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

No comments:

Post a Comment