Ikiwa zimebaki siku 12 kuelekea msimu wa tatu wa CRDB Bank Marathon tarehe 14 Agosti 2022, imeelezwa kuwa jumla ya zawadi za shilingi milioni 100 zitashindaniwa katika mbio hizo zinazotarajiwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 6,000.
Taarifa hiyo imetolewa leo katika hafla fupi iliyokutanisha wadau na washirika wa CRDB Bank Marathon iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nsekela amesema katika mbio za mwaka huu Benki hiyo imefanya maboresho makubwa katika zawadi ili kuongeza ushindani miongoni mwa washiriki, lakini pia kuendana na hadhi ya kimataifa ambayo mbio hizo ilipata mwaka jana.
“Katika mbio ndefu za 42.2km, washindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake watapata shilingi milioni 10 kila mmoja. Washindi hawa pia watapata zawaidi ya kulala usiku mmoja hapa Johari Rotana, pamoja na vocha za zawadi katika duka la Justfit,” alieleza.
Akitoa majumuisho ya zawadi hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa alisema kuwa katika mbio hizo ikiwamo 21.1km, 10km, 5km, na baiskeli 65km washindi 6 wa kwanza watapewa zawadi za fedha taslimu.
Tully aliongezea pia kutakuwa na zawadi kwa makundi maalamu ya wazee, watoto, na wakimbiaji waliovaa kipekee. “Jumla ya zawadi hizi zote zitakazotolewa kwa washindi ni shilingi milioni 100,” alisema Tully.
Katika hafla hiyo, Benki ya CRDB pia ilitambulisha vifaa vitakavyotumika katika msimu wa tatu wa CRDB Bank Marathon ikiwamo medali, fulana, kofia, bib, pamoja na mfuko wa kuwekea vifaa (back-pack), ambazo washiriki wa mbio hizo watapewa.
Kwa upande wa usajili, Nsekela alisema mpaka sasa tayari watu zaidi ya 4,200 tayari wameshajisajili kushiriki mbio hizo. Nsekela alibainisha kuwa kati yao 801 ni wakimbiaji kutoka nje ya nchi, na kutoa rai kwa Watanzania kuchangamkia nafasi zilizobaki.
“Niwashukuru wale wote waliojisajili katika mbio hizi. Kwa wale ambao bado niwasihi kutembelea tovuti yetu ya www.crdbbankmarathon.co.tz kujisajili, mtu binafsi atachangia shilingi 40,000 na washiriki kupitia vikundi ni shilingi 30,000,” alisema.
Aliongezea: “Katika siku hizi chache zilizobaki tungependa zaidi kuona Watanzania wengi wakijitokeza kujisajili na kushiriki kwa wingi kwani hii ni marathon yetu na tungependa pia kuona zawadi hizi zikibaki nyumbani.”
Aidha Nsekela alitumia fursa hiyo kumshukuru Makamu, Dkt. Philip Mpango kwa kukubali kuwa mgeni rasmi kati mbio hizo. Aliongezea kuwa viongozi mbalimbali tayari wameshajisajili kushiriki ikiwamo Waziri wa Michezo, Mohamed Mchengerwa.
Viongozi wengine waliojisajili kushiriki ni Pamoja na Naibu Waziri wa Michezo, Pauline Gekule, Naibu Spika, Mussa Zungu, Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo.
Akiongea kwa niaba ya washirika wa CRDB Bank Marathon, Mkurugenzi wa Mkuu wa Sanlam, Julius Magabe alisema kampuni yao inajivunia kuwa washirika wa CRDB Bank Marathon kutokana na mbio hizo kujikita zaidi katika kuhamasisha watu kusaidia jamii.
“Tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizi zinazowaleta Watanzania kushiriki katika kutatua changamoto katika jamii. Sanlam ni kampuni ambayo inajali afya na mazingira ya watu wake hivyo tunakila sababu ya sisi kushiriki katika mbio hizi,” alisema Magabe.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizo ambazo zinalenga kukusanya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kusaidia gharama za matibabu kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi katika hospitali ya CCBRT, na upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya moyo JKCI.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi akitoa shukrani kwa Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizo ambazo zinazolenga kukusanya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kusaidia gharama za matibabu kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi katika hospitali ya CCBRT, na upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya moyo JKCI.
No comments:
Post a Comment