NAIBU KATIBU MKUU WA MALIASILI NA UTALII, JUMA MKOMI AWATAKA WAHIFADHI KULINDA MALIASILI ZA TAIFA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 30 August 2022

NAIBU KATIBU MKUU WA MALIASILI NA UTALII, JUMA MKOMI AWATAKA WAHIFADHI KULINDA MALIASILI ZA TAIFA

Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi akizungmza na Wahifadhi wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka ambapo amewataka mafunzo watakayoyapata wayatafsiri kwa vitendo.

Baadhi ya Wenyeviti wa Kanda za Kiikolojia wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahifadhi katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka.

Mkurugenzi Msaidizi wa Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na utalii, Juma Mkomi akimuelezea lengo la mafunzo kwa Wahifadhi mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kufungua mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wahifadhi katika nyanja ya Inteligensia, Uchunguzi na Mashtaka.

NAIBU Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amewataka Wahifadhi  kwenda kusimamia jukumu ya msingi la Wizara ya Maliasili na Utalii  ambalo ni kulinda na kuhifadhi maliasili za Taifa ikiwemo Misitu na Wanyamapori.
Mkomi  ameyasema hayo Agosti 30, 2022  Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo yamehudhuriwa na  Washiriki kutoka  Jeshi la Polisi nchini ,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wahifadhi  kutoka TANAPA, NCAA, TAWA na TFS. 
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mkomi amesema Wahifadhi  wana wajibu wa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama  katika kuwabaini majangili wa wanyamapori na Misitu. Amewataka Washiriki hao kuzingatia mafunzo hayo na kwenda kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha Wahalifu wa wanyamapori na misitu wanakamatwa kabla ya kuharibu Maliasili zetu.  
“Mafunzo hayo mtakayopewa yakawe chachu katika kuchagiza utalii hivi sasa  filamu ya Royal Tour imeitangaza vizuri nchi yetu na Watalii wameanza kumiminika nchini kutokana na kazi kubwa mnayofanya ninyi Wahifadhi msingekuwa mmefanya kazi kubwa kulinda wanyamapori watalii wasingekuja kwa sababu kusingekuwa na wanyamapori,” amesema.
Kutokana na jukumu walilonalo la kulinda Maliasili, Naibu Katibu Mkuu, Mkomi amewataka wahifadhi hao kuzingatia mafunzo hayo hususani suala la uchunguzi kwa kujifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea kwenye maeneo ya hifadhi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt. Maurus Msuha  amesema suala la Uhifadhi linakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa Maliasili hivyo  mafunzo hayo yakalete majawabu katika kulinda maliasili.

Pia Dkt. Msuha amesema  mafunzo hayo  yanakwenda kuboresha utendaji kazi kwa kuhakikisha uhalifu wa wanyamapori na Misitu litachochea ufanisi zaidi katika utendaji wa kazi wa kulinda maliasili zetu.

Naye Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Wanyamapori, Robert Mande amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa kukumbushana namna ya kushughulika na waharifu wa wanyamapori wa misitu mara wanapokamtwa.
“Lazima tuhakikishe kuwa tunalinda rasilimali za wanyamapori ili watalii wanavyokuja waweze kuziona na waweze kuwa na usalama,” Mande amefafanua.

No comments:

Post a Comment