MILANGO ya uwekezaji mkoani Ruvuma imefunguka baada ya wawekezaji kwenye sekta ya kilimo kutoka nchini Misri kuwasili mkoani Ruvuma.
Wawekezaji hao wanatarajia kuwekeza katika zao la mahindi ya njano ambapo kwa mwaka wanahitaji mahindi ya njano zaidi ya tani milioni moja.
Akizungumza mara ya kupokea wawekezaji hao, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Mkoa umebahatika kutembelewa wawekezaji toka nchini Misri ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye kilimo cha mahindi ya njano.
Hata hivyo amesema mahindi ya njano ni zao maalum kwa ajili ya kuzalisha vyakula vya Wanyama ambapo wawekezaji hao wameahidi kuleta mbegu ya mahindi ya njano kwa wananchi ili wawe wazalishaji wakubwa wa mahindi hayo.
“Bado tunaendelea na majadiliano na wawekezaji hao kwa kuzingatia sheria za mbegu kwa sababu nchi yetu bado haijaruhusu kupokea mbegu ambazo zimefanyiwa GMO kwa sababu tunalinda zile mbegu zetu za asili tulizonazo’’, alisema.
Amesema mara baada ya kufikia makubaliano na taratibu zote kukamilika itatolewa taarifa kwa wananchi ambapo amewaasa wananchi kuwa tayari kuwapokea wawekezaji wakubwa katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mfasara wa wawekezaji hao kutoka nchini Misri, Bassem Maher Allattia ambaye anatoka Kampuni ya Smart For Import and Export ya jijini Cairo nchini Misri,amesema wametembelea Tanzania kwa lengo la kutafuta mahindi ya njano ambayo watanunua na kupeleka nje ya nchi.
Bassem amesema wamefika Tanzania kwa maelekezo ya Rais wa Misri ambaye amewaagiza kuwekeza Afrika hasa Tanzania ambapo wamedhamiria kununua mahindi ya njano zaidi ya tani milioni moja kila mwaka.
Wawekezaji hao tayari wametembelea wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma zikiwemo, Namtumbo, Tunduru, Mbinga, Nyasa na Songea ambako wamejionea fursa mbalimbali za Uwekezaji katika sekta za kilimo na madini.
Kwa upande wake Mwekezaji Wael Ibrahim Ahmed amesema amefurahi sana kuja kuwekeza katika nchi ya Tanzania yenye watu wakarimu na wenye upendo.
Amesema ushirikiano baina ya Tanzania na Misri utachochea maendeleo makubwa katika nchi zote mbili hivyo kuchangia uchumi wa wananchi.
No comments:
Post a Comment