FURSA ZA MICHEZO NA ZA KIBALOZI ZITUMIKE KUVITANGAZA VIVUTIO VYA NCHI – MHE. OTHMAN - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 3 August 2022

FURSA ZA MICHEZO NA ZA KIBALOZI ZITUMIKE KUVITANGAZA VIVUTIO VYA NCHI – MHE. OTHMAN

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akifurahia Jambo na ujumbe wa Kamati ya Mbio za Kimatiafa za Marathon Zanzibar waliofika kufanya nae mazungumzo kuhusu mashindano hayo ya mbio zinaotarajiwa kufanyika tarehe 07.08.2022, kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza Migombani Zanzibar leo Agost 03, 2022. (Picha na Kitengo cha Habari Ofisi ya Makamu wa Kwanza Wa Rais wa Zanzibar).

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania  nchi za nje kuhakikisha wanazitambua na kuziainisha vyema fursa muhimu zilizoko ili zitumike kuisaidia nchi kiuchumi na kimaendeleo. 

Mhe. Othman ameyasema hayo Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar akizungumza na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Suleiman Haji Sulemain, aliyefika ofisini kwa Makamu kumuaga akielekea kituo chake cha Kazi Mjini New York nchini Marekani.

Amesema kwamba hivi sasa Tanzania kama zilivyo nchi zote dunaini zinazingatia sana kutekeleza Diplomasia ya kiuchumi kwa kukaribisha wawekezaji na mashirikiano ya Kampuni kubwa mbali mbali katika jitihada za kukuza maendeleo hasa katika ulimwengu huu wa Kidijitali.

Mhe.Othman ameeleza kwamba Nchi ya Tanzania inaendelea kufunguka kiuchumi kwa kukaribisha ujuzi na mitaji katika ushirikiano wa uwekezaji ili kuifanya nchi kuweza kusonga mbele kwa kutumia faida na tija ya ushirikiano huo kutoka mataifa na Jumuiya mbali mbali Ulimwenguni.

Aidha amewataka mabalozi pia kujitahidi kuhakikisha ushiriki wa Tanzania unakuwepo katika masuala muhimu kwa kuwasilisha taarifa za masuala muhimu ya Nchi na makampuni mbali mbali na hatimae ziweze kutumika katika kuchangia kukuza uchumi.

Naye Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Suleiman Haji Suleiman, ameeleza kwamba atajitahidi kufuata maelekezo aliyopewa ili kusaidiana kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ikiwemo Taasisi za Kikanda katika kuunganisha na kutumia fursa tofauti zilizopo duninani ili ziweze kuinufaisha Tanzania kwa namna tofauti.

Wakati huo huo Mhe. Othman amekutana na Kamati ya Zanzibar Marathon na kuitaka kuhakikisha kwamba shughuli  za Kimichezo zinatumika katika kuitangaza vyema Zanzibar kwa mambo na vivutio mbali mbali vilivyopo nchini kwa vile yanaweza kuleta tija kubwa kwa kuchangia kukuza uchumi kupitia sekta ya Utalii kama zinavyofanya nchi nyengine nyingi Duniani.

Amesema kwamba Zanzibar ina vivutio vingi vya kihistoria ambavyo havijafahamika kwa wageni kwa kuwa havijatangazwa vyema na kwamba marathon za kimataifa zinaweza kutumika kama ni fursa ya kuitangaza zaidi na nchi kunufaika na vivutio mbali mbali vya historia  vilivyopo.

Pia ameipongeza Kamati hiyo kwa kuendeleza mbio  hizo za marathon Zanzibar na kuongeza washiriki zaidi ambao watachangia kuitangaza zaidi Zanzibar kiutalii katika  nchi mbali mbali duniani.

Mapema Msemaji wa Kamati hiyo Bw. Farouk Karim, ameeleza kwamba mbio za mwaka huu zimepanua wigo wake zaidi kwa kuongeza  washiriki katika kukimbia kwa  mbio za kilomita tano, kumi na 21 zikiwemo mbio za baiskeli  za zaidi ya kilomita 38.

Amefahamisha kwamba mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Jumapili Agost 07,  zinatanguliwa na matamasha mbali ,mbali ili kuwapa nafasi wenyeji na watalii mbali mbali kutambua shughuli hiyo  ambayo ni  muhimu katika kuitangaza Zanzibar kiutalii katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua uchumi.

No comments:

Post a Comment