SERIKALI, LIONS CLUB YAKABIDHI CHUO CHA UFUNDI MSANDAKA MKOANI KILIMANJARO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 29 July 2022

SERIKALI, LIONS CLUB YAKABIDHI CHUO CHA UFUNDI MSANDAKA MKOANI KILIMANJARO

Majengo ya Chuo cha Ufundi Msandaka yanvyoonekana baada ya ufunguzi uliofanywa na Mkurugenzi wa Elimu Mahitaji Maalum Tanzania Dkt. Magreth Matonya.

Mkurugenzi wa Elimu Mahitaji Maalum Tanzania Dkt. Magreth Matonya akishuhudia wanafunzi viziwi wenye ujuzi katika fani ya ushonaji wanavyofanya.

Ufunguzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Msandaka ulivyofanywa.

 Wanafunzi Viziwi wa Shule ya Msandaka wakiimba wimbo mbele ya wageni washiriki wa hafla ya ufunguzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Msandaka.

Na Kija Elias, Moshi

SERIKALI  kwa kushirikiana na wahisani wa Lions Club of Moshi Kibo pamoja na Lions club of Belgium  wamekabidhi Chuo cha Ufundi Stadi (VTC) kwa shule ya watoto wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) Msandaka, iliyopo Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza jana katika hafla fupi ya kukabidhiwa kwa chuo hicho, Mkurugenzi anayeshughulikia watoto wenye mahitaji maalumu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Magreth Matonya, alisema chuo hicho ni cha kwanza kitaifa ambapo hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni mikakati ya serikali kuhakikisha watu wenye mahitaji maalumu  wanapata ujuzi utakao wawezesha kujikwamua kiuchumi.

Katika hotuba yake Dkt. Matonya aliwashukuru wahisani kwa mchango mkubwa walioutoa kufanikisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Msandaka, kwani kuna watoto viziwi wanaofikishwa shuleni wakiwa na umri mkubwa ambao hawawezi kuingia madarasa ya kawaida, wanatakiwa kwenda kwenye madarasa ya ujuzi, kwa hiyo wakifika shuleni serikali inawabaini na kugundua ujuzi walionao baada ya hapo wanawapeleka kwenye madarasa ya ufundi.

“Tumekuta wanafunzi hawa wanajifunza ufundi cherehani, wanajifunza ufundi seremala na ushonaji, tumeona wanatengeneza viti vizuri, stuli nzuri lakini wana vifaa vya kisasa ambavyo wamepewa na wahisani kutoka Lions Club International, kituo hiki ni muhimu sana,” alisema Dkt. Matonya.

Aidha Dkt. Matonya alisema uwepo wa chuo hicho kilichojengwa kwa zaidi ya shilingi mil. 700 utaifungua jamii kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kwa kuwa wapo watoto viziwi ambao hawawezi  kufuata mifumo ya elimu ya kawaida, elimu ambayo ni ya mfumo rasmi, hivyo uwepo wa chuo hicho cha ufundi  utawawezesha watoto hao kupata ujuzi utakaowasaidia katika suala la kujikimu  kimaisha pindi watakaporudi majumbani.

Dkt. Matonya aliongeza kuwa wapo watoto  wengine waliomaliza kidato cha nne na hawakufanya vizuri  lakini wamejiunga na  chuo hicho  cha ufundi na wanajifunza kwa bidii na hivi sasa wanafanya vizuri.

Sambamba na hilo Dkt. Matonya aliwashukuru wahisani kwa kutengeneza mabweni ya kuishi kwaajili ya watoto viziwi  kutokana na mazingira hatarishi ambayo watoto hao wanapitia.

"Kunavitu vingi sana wanavyokumbana navyo wanapokua njiani kuja shuleni, lakini pia zipo familia ambazo bado haziwajali  watoto wenye mahitaji maalum kiasi kwamba wanawanyanyapaa na kuwaficha, lakini wanapokua bweni  wanakua na muda mrefu  wa kujisomea kuliko wanapokua  nje na shule,"alisema Dk. Matonya.

Mkuu wa shule ya Viziwi Msandaka Rosada Shayo, alisema sababu kubwa ya kuanzisha ujenzi wa chuo hicho ni baada ya kubaini kuwa wanafunzi wao wanapomaliza shule ya msingi na kujiunga na sekondari wanapofika kidato cha pili hurudishwa nyumbani kutokana na matokeo mabaya hivyo kuangukia tena katika changamoto.

Awali akitoa  taarifa juu ya ujenzi wa Chuo hicho cha Ufundi Stadi (VTC) Mwenyekiti wa Lions Club of Moshi Kibo Sarah Mandara, alisema ujenzi wa chuo hicho umegharimu kiasi cha shilingi milioni 700  ambazo zimetumika kukamilisha ujenzi  huo uliojumuisha vyumba sita vya madarasa pamoja na karakana kwaajili ya watoto kujifunzia.

“Jumuiya ya kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali ya Lions Club of Moshi Kibo, imefadhili ujenzi wa chuo hiki cha Ufundi Stadi (VTC) katika shule ya viziwi Msandaka,  iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 700, na leo hii tumekikabidhi kwa Serikali ili watoto hawa waweze kufikia malengo yao,”alisema Sarah.

Hata hivyo Profesa Jerome Sheridan kutoka Ubelgiji alisema elimu ndiyo kitu muhimu cha kuwasaidia wenye mahitaji maalum kutokana na changamoto wanazopitia.

“Ndugu wanafunzi, chuo chenu cha ufundi stadi sasa ni halisi, kwanini tumefanya hivi? kwasababu tuna imani nanyi…licha ya changamoto lakini mnaweza kuzikabili endapo mtasoma katika chuo hiki,” alisema Prof. Sheridan.

Aidha Profesa Sheridan alisisitiza kuwa Chuo cha Ufundi Stadi Msandaka kitaenda mbali zaidi ya kujihusisha na kilimo ili kuwajengea uwezo zaidi wanafunzi wenye mahitaji maalum.

“Kilimo ni muhimu lakini chuo hiki cha ufundi kitaenda mbali zaidi ya kilimo kwa kuwapatia ujuzi mwingine ili wajitegemee katika maisha yao,” alisema Prof. Jerome.

Awali Mratibu wa Viziwi Tanzania Selemani Chamshama, alisema miaka ya hivi karibuni mtazamo wa jamii kuhusu wanafunzi wenye uhitaji maalum umebadilika na kuwa chanya ukilinganisha na miaka mingi iliyopita.

“Chuo hiki ni adimu kwa nchi yetu. kama mnavyokumbuka miaka ya nyuma jamii ilikuwa haina uelewa mkubwa juu ya wanafunzi viziwi lakini sasa kumekuwa na uelewa mkubwa juu ya wanafunzi wenye ulemavu hususani viziwi,” alisema Chamshama.

Aidha Gavana wa Wilaya wa Lions Club aliyepo Tanzania Mustansir Ghulam Hussein alitoa shukrani zake za dhati kwa Lions Club wa Ubelgiji kwa kufanikisha ujenzi wa chuo hicho.

“Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kutuunga mkono, pamoja tumesimama na pamoja tumeuungana…ndoto tuliyoota pamoja sasa imekuwa halisi,” alisema Ghulam Hussein.

Kwa upande wake Katibu wa Lions Club of Moshi Kibo, Inderjeet Rehal  kwa jina maalufu ‘NITU’ alisema, “Malengo ya kuanzishwa kwa Chuo cha Ufundi Stadi ni kuwezesha vijana hao wanapomaliza darasa la saba waweze kuishi maisha mazuri baada ya kumaliza mafunzo ya chuo.

“Tumegundua watoto hususani wa kike wanapomaliza darasa la saba wengine wanatupwa, wanapata ujauzito na kuepukana mambo kama haya tukaona tuwawezeshe wapate elimu ya Ufundi, ili waweze kujiendeleza kielimu zaidi,” aliongeza Nitu.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa kituo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe alisema kuwa kituo hicho kitawasaidia watoto viziwi kupata ujuzi mbalimbali ambao utawawezesha kujiajiri na kuepuka kuwa tegemezi kwa jamii inayowazunguka.

No comments:

Post a Comment