OFISI YA ARDHI MKOA WA SINGIDA YAANZA KUSIKILIZA KERO ZA MIGOGORO YA ARDHI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 25 July 2022

OFISI YA ARDHI MKOA WA SINGIDA YAANZA KUSIKILIZA KERO ZA MIGOGORO YA ARDHI

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza akizungumzia kuhusu ofisi ya Ardhi Mkoa wa Singida ilivyoanza leo Julai 25,2022 kusikiliza kero za migogoro ya ardhi ya wananchi kwa kila halmashauri ili ziweze kutatuliwa.

Wananchi wa Mkoa wa Singida wakiandika majina baada ya kufika Ukumbi wa Zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida kupeleka kero zao zinazohusu ardhi.
Afisa Msajili Msaidizi, Godilize Jerady (kulia) akikabidhi fomu kwa ajili ya kupokelea nyaraka zinazohusu usajili kutoka kwa mmoja wa wananchi aliyefika kupeleka maombi ya kubadilishiwa jina kwenye kitambulisho cha Taifa akiwa ameongozana na mama yake.

Mwananchi Maulid Ndui (kushoto)akitoa akielezea kero yake inayohusu ardhi kwa maafisa ardhi waliokuwa wakipokea kero mbalimbali.

Mkazi wa Manispaa ya Singida, Khalifa Matali (kulia) akitoa kero yake.


Mkazi wa Puma,  Abdillah Said akielezea kero yake.

Mkazi wa Sabasaba Manispaa ya Singida, Zuhura Salum akielezea kero yake.

Mkai wa Dung;unyi wilayani Ikungi, Mathew Mpaji akizungumzia kero yake. 

Na Dotto Mwaibale, Singida

OFISI ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Singida imeanzisha utaratibu wa kusikiliza kero za migogoro ya ardhi ya wananchi kwa kila halmashauri ili ziweze kutatuliwa.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, akizungumza leo Julai 25, 2022 alisema utaratibu huo ambao utakuwa endelevu unalenga kupunguza au kumaliza kero za migogoro ya ardhi ambayo baadhi zimekaa muda mrefu bila kutatuliwa..

Hoza alisema maofisa ardhi wa halmashauri zote wahakikishe wanatenga muda wao wa kushughulikia kero za ardhi katika siku maalum zilizopangwa na kuzitatua.

Alisema hakuna sababu kwa wananchi kusubiri hadi ziara za viongozi wakuu ndipo watoe malalamiko yao ya kero ya migogoro ya ardhi hivyo watumie muda wao kupeleka migogoro yao kwa maafisa ardhi ili iweze kutatuliwa.

Katika siku ya kwanza ya zoezi la kusikiliza kero za migogoro ya ardhi watu wengi wamejitokeza katika ofisi ya zamani ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida vijijini kwa ajili ya kupeleka kero zao kwa maafisa ardhi.

Baadhi ya wananchi waliofika kutoa kero zao za migogoro ya ardhi iliyotofautiana akiwepo Maulid Ndui,  Abdillah Said kutoka Puma wilayani Ikungi, Khalifa Matali kutoka Manispaa ya Singida, Mathew Mpaji kutoka Dung'unyi wilaya ya Ikungi na Zuhura Salum kutoka maeneo ya Sabasaba Manispaa ya Singida walimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhimiza watendaji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuacha kukaa ofisini badala yake watoke kwenda kusikiliza kero mbalimbali zinazotokana na migogoro ya ardhi nchi nzima.

Aidha wananchi hao walimpongeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza na watendaji wa ofisi hiyo kwa kutekeleza agizo la Serikali kwa kuanza kuwasikiliza wananchi wenye kero za migogoro ya ardhi ili ziweze kutatuliwa haraka iwezekanavyo.

Wananchi hao walisema hatua hiyo imewapunguzia adha ya kusafiri kwenda Dar es Salaam na Dodoma kwa ajili ya kupeleka malalamiko yao ambapo hapo awali walikuwa wakipote muda na fedha wakati wa kushughulikia mogogoro hiyo.

“Kwa kweli niipongeze wizara hiyo na Kamishna Hoza kwani hii walioichukua itasaidia kuwafanya watu wengi wenye migogoro ya ardhi ambao walikuwa hawana uwezo kuja kwa wingi kuleta kero zao,” alisema Zuhura Salum.

Aidha Zuhura Salum aliiomba ofisi ya ardhi Mkoa wa Singida kuongeza siku za kusikiliza migogoro hiyo kutoka siku moja na kuwa wiki moja kutokana na wingi wa wananchi wenye malalamiko mbalimbali yanayohusu ardhi.


No comments:

Post a Comment