Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha TLP, Augustino Mrema. |
Na Thobias Mwanakatwe
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha TLP, Augustino Mrema, amesema uteuzi na
mabadiliko ya wakuu wa mikoa uliofanya na Rais Samia Suluhu Hassan iwe chachu kwa walioteuliwa kufanya kazi kwa bidii
kumsaidia rais katika kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi nchini.
Akizungumza jana kwa simu akiwa jijini Dar es Salaam, alisema rais
anapofanya mabadiliko ya viongozi dhamira yake kuu ni kutaka kuona wasaidizi
wake wanamsaidia katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mrema ambaye ni mwanasiasa mkongwe ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa
ikiwano ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema rais
tuliyenaye anapenda kuona wasaidizi wake wanaleta mabadiliko ya kimaendeleo
katika maeneo aliyowateua.
"Viongozi waliobahatika kuteuliwa cha msingi wakishaanza kutekeleza
majukumu yao wachape kazi kuwaletea maendeleo wananchi maana dhamira ya rais ni
kuiona Tanzania inakuwa nchi yenye watu wake wenye maendeleo makubwa,"
alisema Mrema.
Mrema aliongeza kuwa mara nyingi watu wanapoteuliwa kushika nyadhifa
mbalimbali za uongozi wanafurahia badala ya kwenda kufurahia unapokuwa
umesaidia kuleta mabadiliko ya maendeleo kwenye eneo ulilopangiwa.
Alisema walioachwa katika uteuzi huu hawana sababu ya kujisikia wanyonge
kwani mchango wao walioutoa wakiwa viongozi unatambulika kwani uongozi ni
kupokezana vijiti.
"Mimi nilikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani leo hii si niko benchi nafasi
ameishika mwingine, na kwenye hizi kazi ukifanya vizuri utakumbukwa daima kwa
uwajibikaji uliotukuka na heshima utakuwa nayo mbele ya jamii kama ikivyo
kwangu mimi," alisema Mrema.
Mrema alisema moja ya majukumu ya Mkuu wa mkoa ni pamoja na kuhakikisha
mkoa wako unakuwa na makusanyo ya mapato na kuzuia rushwa na upotevu wa mapato
kwenye halmashauri zilizopo kwenye mkoa husika.
Aliongeza kuwa katika siku za karibu tumekuwa tukishuhudia na hata katika
ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) halmashauri
nyingi zikikumbwa na kashfa ya ubadhirifu wa mapato na wakuu wa mikoa wapo
lakini hawachukui hatua kwa watendaji wao wa chini.
Mrema alisema sio jambo lenye afya kiongozi wa kitaifa anapofanya ziara
katika mkoa wako na kuibua suala la ubadhirifu wa mapato wakati wewe kama Mkuu
wa Mkoa upo na haukufanya jambo lolote kuchukua hatua kudhibiti haki hiyo.
No comments:
Post a Comment