MKUTANO WA KIMATAIFA WA ELIMU BORA, KUFANYIKA AGOSTI 17-19, 2022 DAR - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 22 July 2022

MKUTANO WA KIMATAIFA WA ELIMU BORA, KUFANYIKA AGOSTI 17-19, 2022 DAR


Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga akizungumza na vyombo vya habari leo juu ya Mkutano wa Kimataifa wa Elimu Bora unaotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 17 hadi 19, 2022 jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga akisisitiza jambo kwa wanahabari leo juu ya Mkutano wa Kimataifa wa Elimu Bora unaotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 17 hadi 19, 2022 jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) unatarajia kuwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka nchi kadhaa barani Afrika kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Elimu Bora utakaoanza Agosti 17 hadi 19, 2022 jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania kujadili masuala anuai ya elimu.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga amesema malengo mahususi ya mkutano huo ni pamoja na Kutambua na kujadili mustakabali wa elimu kwa pamoja, Kubadilishana uzoefu ndani na nje ya Tanzania kuhusu mambo mazuri yanayofanyika kwenye sekta ya elimu na Kusambaza matokeo ya utafiti kuhusu tafiti mbalimbali za elimu.

Bw. Wayoga alisema lalengo mengine ni kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bunifu za ugharamiaji wa elimu - mitazamo ya kimataifa/ na ya ndani, kutoa fursa kwa wadau wa elimu kuonesha juhudi/afua/kazi zao katika sekta a pia Kushawishi mabadiliko ya sera ya elimu katika mwelekeo sahihi kwenye karne ya 21.

"...Matarajio yetu ni kuwa mwishoni mwa mkutano washiriki wataweza: Kubuni na kutoa maamuzi kuhusu mbinu bunifu za kuboresha elimu, Kupata uzoefu, teknolojia na utaalamu kuhusu usimamizi bora wa sekta ya elimu, Kuboresha ufumbuzi endelevu wa ugharamiaji wa elimu, pia kushiriki katika Mikutano na mijadala ya mkutano pamoja na Kupata suluhu zinazowezekana kushughulikia suala la ubora na umuhimu wa elimu," amesema Bw. Wayoga akizungumza na wanahabari.

Hata hivyo ameongeza kuwa TENMET inatoa rai kwa wadau wa elimu ndani na nje ya nchi yetu ya Tanzania kushiriki katika mkutano huo, kwani utaendeshwa kwa njia ya mijadala, ambapo mada mbalimbali zinazohusiana na za kielimu zitajadiliwa.

Mratibu wa Taifa wa TEN/MET, Bw. Wayoga akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam.

Alizitaja mada zitakazowasilishwa ni pamoja na Lugha za Kiafrika katika kufundishia na kujifunzia, Kufikiria upya Mustakabali wa Elimu, Kufikiria upya Mustakabali wa Pamoja; Mkataba mpya wa Kijamii wa Elimu (Ripoti ya UNESCO) na Uboreshaji Teknolojia ya Kufundishia na Kujifunzia - Kupunguza Pengo la Kidijitali katika Elimu- muktadha wa Afrika.

Mada zingine ni Kuzuia muongo uliopotea - Hatua za haraka za kupunguza athari mbaya za UVIKO-19 kwa watoto na vijana- (RIPOTI YA UNICEF), Kuimarisha Mifumo ya data ya Elimu nyakati za dharura na migogoro- Masomo na ubunifu pamoja na Uboreshaji wa sera ya elimu ikiwa ni pamoja na mitaala na stadi za kazi iatakayowasilishwa na WIZARA YA ELIMU.

"...Mkutano huu  unategemea kuleta washiriki kutoka  ndani na nje ya nchi  na utaendeshwa kwa njia mbili, kwa washiriki kuhudhuria mubashara, na  wengine kwa njia ya kimtandao. Kwa maoni na taarifa zaidi za namna ya kushiriki, tafadhali tembelea tovuti yetu www.tenmet.or.tzna mitandao yetu ya kijamii kupitia Instagram(@tenmet), Facebook na Twitter (@ten_met)," alisisitiza Mratibu huyo wa Taifa TEN/MET.

Mkutano huo wa Kimataifa wa Elimu Bora hutoa fursa kwa wadau wa elimu ikiwepo serikali, watunga sera, vyuo vikuu,wanafunzi, watafiti, taasisi za elimu, mashirika ya umma na binafsi, Washirika wa Maendeleo (Development Partners) pamoja na wadau mbalimbali wa elimu nchini kujadili hali ya ubora wa elimu kwa nia ya kuboresha utoaji wake.

No comments:

Post a Comment