KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU ATEMBELEA BODI YA MIKOPO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 22 July 2022

KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU ATEMBELEA BODI YA MIKOPO

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael akisalimiana na Watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu HESLB wakati wa ziara yake aliyoifanya Julai 21, 2022 katika Ofisi za Makao Makuu ya HESLB Tazara Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru akimtambulisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael kwa watumishi mbalimbali wa HESLB, wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za Makao Makuu ya HESLB, Tazara Jijini Dar es Salaa Julai 21, 2022.

Na Mwandishi Wetu, DAR

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael ameipongeza Menejimenti na Watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa utendaji kazi wenye matokeo, tija na ufanisi.

Dkt. Francis amesema hayo Julai 21, 2022 wakati wa ziara yake ya kutembelea HESLB na kujitambulisha kwa menejimenti na watumishi wa taasisi hiyo tangu kuteuliwa kwake hivi karibuni na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuongoza Wizara hiyo.

Nimekuja kuwatembelea na kujitambulisha, niwapongeze kwa kazi mnayoendelea kufanya katika kuwahudumia wanafunzi wahitaji na wanufaika wa mikopo, mmeonyesha kasi inayotakiwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwahudumia wananchi”. 

Aidha  Dkt. Francis amesema ziara hiyo ameifanya kwa malengo maalum ya kukutana na watendaji na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ili kuhimiza utendaji kazi na kueleza kufurahishwa kwake na taarifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB iliyoonesha utayari katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru ameishukuru Wizara kwa kuiwezesha HESLB ikiwemo kutenga bajeti ya kutosha katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria ikiwemo utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na kusimamia urejeshaji.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuiwezesha HESLB kuitengea bajeti ya kutosha kwa wanafunzi wahitaji, tunaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufikia malengo na matarajio yaliyowekwa na Serikali katika kuwahudumia wananchi,” amesema Badru.

Aidha katika hatua nyingine, Dkt. Francis pia alikutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa HESLB kwa ajili ya kujitambulisha na kusikiliza maoni yao ambapo amesema akiwa kiongozi wa Wizara hiyo atahakikisha atawafikia na kuwasikiliza watumishi wote waliopo katika kada za chini.

“Sote tumetoka huko mlipo, nikiwa kama Kiongozi wenu nipo tayari kuwasikiliza ili kuweza kufahamu changamoto zilizopo katika Wizara na taasisi zake ili kuhakikisha kuwa tunafanya kazi kwa pamoja ili kuweza kuleta tija iliyokusudiwa”.

Akiwasilisha salamu za Wafanyakazi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Ushauri Habari na Utafiti (RAAWU) Tawi la HESLB, Daudi Elisha amemshukuru Dkt. Francis kwa kutenga muda wa kukutana na watumishi wa kada za chini kwani kitendo hicho kimedhihirisha kutambua nafasi ya watumishi wote katika utendaji na utumishi wa umma.

No comments:

Post a Comment