BALOZI wa Tanzania nchini Uingereza Dkt. Asha-Rose Migiro leo Julai 25, 2022 ametembelea kambi ya wanamichezo wa Tanzania wataoshiriki kwenye Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola iliyopangwa kuanza Julai 28, 2022, na kuwatakia kila la heri kwenye michuano hiyo inayoshirikisha jumla ya nchi 72.
Dkt. Migiro, ambaye alimuwakilisha kiongozi wa msafara Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa katika hafla ya kukaribisha rasmi nchi zinazoshiriki, alitoa pia salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wanamichezo hao, akisema kiongozi huyo wa nchi na Watanzania wote kwa ujumla wana imani kubwa na wanamichezo hao kwamba watafanya vizuri kwenye mashindano.
"Macho na masikio ya Mhe. Rais na ya Watanzania wote yako hapa Birmingham na wote wanawategemea kwamba mtafanya vyema kwenye michezo hiyo hivyo mjitume na kupigania heshima ya nchi kwa nguvu zote, huku mkidumisha amani, nidhamu na furaha wakati wote mtaokuwa hapa", alisema.
Kwenye michezo hiyo Tanzania inawakilishwa na wanariadha tisa, mabondia watatu, wacheza judo wawili na waogeleaji wawili. Wachezaji wote wameshawasili Birmingham isipokuwa wanariadha wa marathon ambao walikuwa kambini Arusha na wanatarajiwa kuwasili siku tatu kabla ya michuano kuanza.
No comments:
Post a Comment