MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema Serikali itahakikisha inaandaa mipango bora ya kukuza Sekta ya Elimu ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sasa ulimwenguni yanayotegemea sana taaluma za ufundi, sayansi na teknolojia.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Juni 1,2022 kisiwani Pemba katika ziara yake maalum ya kikazi ambayo imejumuisha pia ukaguzi wa miradi mbalimbali ya kuendeleza sekta ya elimu hapa Visiwani.
Amesema kuwa ni wajibu wa Serikali kwa sasa kuwekeza katika kufanikisha elimu itakayotoa wasomi bora wa kada tofauti zikiwemo za ufundi, ambapo hilo litawezekana kwa mamlaka zinazosimamia sekta hiyo kuandaa mipango makini.
Mhe. Othman ambaye katika ziara hiyo ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, alikagua Ujenzi wa Madarasa Matano katika Skuli ya Mizingani, kukagua maendeleo ya Skuli ya Pindua, Kituo cha Elimu Mjumuisho cha Pujini na Skuli ya Sekondari ya Madungu, zote katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Kabla ya hapo Mhe. Othman alipita kusalimia, kuwafariji wahusika na kutembelea Mabweni ya Skuli ya Ufundi ya Kengeja, ambayo yaliteketea vibaya kwa kuungua moto, katikati ya Mwezi wa Mei, 2022.
Kufuatia tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Bw. Mattar Zahor Masoud, aliiarifu hadhira hiyo kwamba tayari ameshapokea Ripoti ya Uchunguzi kupitia Kamati aliyoiunda mara tu baada ya ajali hiyo.
Ziara hiyo imewajumuisha Viongozi mbali mbali wa Serikali, Jamii, Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Vyama vya Siasa, Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Pemba, Maafisa Wadhamsi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment