KIPUPWE 2022: SEKTA MBALIMBALI ZASHAURIWA KUCHUKUA TAHADHARI YA VIPINDI VYA BARIDI NA UPEPO MKALI VINAVYOWEZA KUJITOKEZA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 1 June 2022

KIPUPWE 2022: SEKTA MBALIMBALI ZASHAURIWA KUCHUKUA TAHADHARI YA VIPINDI VYA BARIDI NA UPEPO MKALI VINAVYOWEZA KUJITOKEZA

 

Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa - TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa Kipupwe unaoanzia Mwezi Juni hadi Agosti (JJA) 2022. Taarifa hiyo imeelezea athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, alisisitiza sekta mbalimbali kuchukua tahadhari za vipindi vya baridi na upepo mkali vinavyoweza kujitokeza nchini.

“Katika kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti, 2022 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi ya nchi, vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa mwezi Juni na Julai huku vipindi vya baridi kali vikitarajiwa katika maeneo yenye miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi, hivyo ni vyema sekta mbalimbali kuchukua tahadhari ya athari zinazoweza kujitokeza”. Alisisitiza Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a aliongezea kuwa hali ya joto la bahari la wastani hadi chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la bahari, kusini-mashariki mwa bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) hali inayotarajiwa kusababisha ukavu katika msimu huo, japo upepo unaotarajiwa kuvuma kutoka kusini mashariki na mashariki unaweza kuleta unyevunyevu kutoka Bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na pwani ya kaskazini (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani). 

Aidha, jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza pamoja na kuzingatia tahadhari za upepo mkali zitakazotolewa na TMA pale zitakapojitokeza.

Kwa taarifa zaidi tembelea; www.meteo.go.tz

https://www.instagram.com/p/CeRh-xrN-m8/?igshid=MDJmNzVkMjY=

No comments:

Post a Comment