Na Lusungu Helela
KATIBU Mkuu, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan ( JICA), Bw. Ara Hitoshi kuhusu kuimarisha ushirikiano baina ya JICA na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Miongoni mwa masuala waliyojadili ni pamoja na kutoa fursa za mafunzo kwa watumishi pamoja na maombi ya vibali vya ajira kwa raia wa kutoka Japan wanaokuja kufanya kazi nchini katika miradi ya Serikali katika Utumishi wa Umma ambapo fursa hiyo huwasaidia Wazawa kubaki na ujuzi unaoweza kutumika hata baada ya miradi ya maendeleo kukamilika.
Aidha, viongozi hao wamepongeza juhudi za ushirikiano wa nchi hizo mbili unaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shigeru Ishiba.
Akizungumza kwenye kikao hicho Katibu Mkuu Mkomi ameishukuru JICA kwa kuendelea kutoa ufadhili masomo wa elimu ya juu kwa Watanzania hususan watumishi wa umma huku akisisitiza kuwa ushirikiano baina pande mbili ni wa kihistoria na utaendelea kuimarika wakati wote katika masuala ya elimu na utumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment