KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzanai (TAA), kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa uzio katika kiwanja cha ndege cha Mwanza ili kuongeza usalama wa kiwanja hicho.
Akizungumza jijini Mwanza mara baada ya kukagua mradi huo ambao umejengwa na Kampuni ya M/s Mumangi Trans & Construction, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ,Mhe. Selemani Kakoso, amesema kukamilika kwa hatua hiyo kutapunguza matukio ya ajali ambazo zimekuwa zikiripotiwa kiwanjani hapo.
“Niipongeze sana Serikali kwa kutoa fedha na kukamilisha mradi huu, maana kulikuwa na matukio ya ajali za wanyama na binadamu na nina imani kwa sasa hatutasikia tena matukio ya ajali", amesema Mwenyekiti Kakoso.
Mwenyekiti Kakoso ameitaka TAA kuhakikisha inaweka mipaka katika maeneo ya viwanja vyao vyote nchini na kuvitafutia mapema hati miliki ili kuepuka uvamizi na kupunguza migogoro kwa wananchi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege.
“TAA mna maeneo makubwa sana kwenye viwanja lakini havina hati miliki mfano Sumbawanga, Mtwara, Songea na maeneo mengine na wananchi wanasogea taratibu msipokaa sawa mtajikuta mnapelekwa mahakamani na kiwanja ni cha kwenu", amefafanua Mwenyekiti Kakoso.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amesema Serikali imejipanga kutekeleza miradi ya maboresho kwa kiwanja cha ndege cha Mwanza ili kuupa hadhi uwanja huo kulingana na taratibu za usafiri wa anga.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Hamisi Amiri, amesema ujenzi wa uzio kwa sasa umekamilika kwa asilimia mia moja na umegharimu takribani bilioni mbili.
Mkurugenzi Amiri ameongeza kuwa ujenzi wa uzio umezingatia viwango vya sasa vya Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), ili kuendana na hadhi na kiwanja hicho.
No comments:
Post a Comment