Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta vya Ujenzi) Balozi Aisha Amour. |
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta vya Ujenzi) Balozi Aisha Amour amewataka madereva wa sekta hiyo kuwa mfano wa kuigwa kwa kuhakikisha wanasimamia vema sheria za usalama barabarani.
Alitoa rai hiyo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na baadhi ya watumishi wa sekta hiyo kwa lengo la kufahamiana, kueleza changamoto zinazowasibu, kupokea maoni kutoka kwao pamoja na kuwaeleza matarajio yake na namna ya kuboresha utendaji kazi wao.
"Nimeona tukutane tuangalie namna bora ya kuboresha utendaji kazi ili tuweze kwenda pamoja katika utekelezaji wa majukumu kwa weledi," alisema Balozi Aisha.
Katika kikao hicho, Balozi Aisha alisema sekta hiyo ambayo ina kitengo kinachosimamia mambo ya usalama, madereva wake wanapaswa kuhakikisha wanaheshimu alama za usalama barabarani zilizowekwa hususani wakati wanapoyapita magari mengine.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Aisha aliwataka madereva hao kupima afya zao mara kwa mara hususani macho na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Alisema endapo dereva atajibaini ana tatizo la kiafya akiwa safarini atoe taarifa badala ya kuendelea kuendesha chombo cha moto.
Aidha, aliwataka watumishi hao kuwa mabalozi wa Wizara kwa kutoa taarifa wanapokuta kuna uharibifu wa miundombinu inayosimamiwa na sekta hiyo.
Balozi Aisha alisema: "Kama mtumishi wa Sekta ya Ujenzi anakuta sehemu kuna shimo barabarani au alama za barabarani zimeondolewa atoe taaarifa haraka ili ziweze kurejeshwa na kutohatarisha maisha ya watumiaji wengine wa barabara”.
Katika mkutano huo Balozi Aisha alikutana na watumishi wa kada nne zilizopo katika sekta hiyo pamoja na wakuu wa idara na vitengo.
No comments:
Post a Comment