Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Trees for the Future Tanzania yenye makao yake makuu mkoani Singida imetoa miche ya miti 2000 kwa ajili ya kuboresha mazingira na kuufanya mkoa huo kuwa wa kijani.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti kimkoa lililofanyika eneo la maziwa ya Kindai na Munang lililoratibiwa na Taasisi hiyo lenye lengo la kuhimiza watanzania kuongeza juhudi katika shughuli za uhifadhi wa mazingira Msimamizi wa miradi wa Taasisi hiyo Veliksi Haji alisema shabaha ya taasisi hiyo ni kutunza mazingira.
Alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na mambo mengine inajihusisha na uhamasishaji wa kilimo endelevu kwa kutumia miti wameazimia kupanda takribani idadi ya zaidi ya miti milioni tatu ambayo ina uwezo wa kustahimili hali ya hewa ya eneo husika.
Haji alisema mazingira yanaharibiwa sana kutokana na shughuli za kibinadamu kama kukata miti kwa ajili ya kilimo, kujengea,malisho ya mifugo na shughuli mbalimbali imepelekea maeneo mengi kuwa wazi na kuharibu uoto wa asili hivyo wanashirikiana na uongozi wa Mkoa wa Singida kama juhudi zao za kuhamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi ili waweze kurudisha uoto wa asili na hali ya hewa kurudi katika hali yake ya kawaida.
"Miaka ya nyuma Singida ilikuwa na mvua za kutosha na vyanzo vya maji vilikuwa vingi lakini sasa hali hiyo haipo tena ndio maana Taasisi yetu imekuwa ikifanya kazi ya kuhamasisha upandaji wa miti" alisema Haji.
Alisema katika kutekeleza malengo yake ya kupanda miti taasisi hiyo inawawezesha kifedha wadau wa maendeleo mbalimbali wanaojihusisha na shughuli za za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira nchini ikiwemo Magereza Tanzania kupitia Gereza la Uyui-Tabora, Ilagala-Kigoma, Msalato-Dodoma, Manyoni-Singida na Gereza la Shinyanga.
Aidha alisema taasisi hiyo inasaidia asasi za kiraia zinazofanyakazi na wakulima ambazo ni ADESE na WAENDELEE za Mkoa wa Singida, TaDeCaO na Frontie Friends of Environment za Mkoa wa Tabora, Women Against Poverty ya Mkoa wa Dar es Salaam, Twitange ya Mkoa wa Iringa, Environment Develepment Group na Life Securing and Relief Services za Mkoa wa Shinyanga na Friends of Lake Tanganyika ya Mkoa wa Kigoma na kuwa kwa kipee taasisi hiyo inashirikiana na Clinton Development Initiative (CDI) iliyoko Mkoa wa Iringa na HELVETAS ya Singida.
Alisema katika Mkoa wa Singida wanafanya kazi katika Halmashauri 4 ambazo ni Ikungi, Iramba, Mkalama na Singida.
Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Singida Mjini Mhandisi Paskas Muragili kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Singida Dk. Binilith Mahenge aliagiza Manispaa ya Singida kuhakikisha inawakamata watu wote watakaoacha mifugo yao ikizurura hovyo na kusababisha uharibifu wa mazingira kwa namna yoyote.
" Ninaagiza mazingira yatunzwe na mifugo isiruhusiwe kuzurura hovyo-hivyo naagizawekeni utaratibu mzuri na muwe na tabia ya kupanda miti na kuitunza ili iwe endelevu kwa kizazi cha sasa na baadae" alisema Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili kwa niaba ya mkuu wa mkoa"
Katika hatua nyingine Dk. Mahenge aliagiza kila kaya mkoani hapa kuhakikisha inalima ekari isiyo pungua moja ya zao la mtama aina ya serena ili kukabiliana na uhaba wa chakula ambao utaweza kutokea kutokana na changamoto zilizopo za mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa upande mwingine, Wizara ya Maji kupitia ofisi yake ya Bodi ya Maji Bonde la Kati ambayo imepewa dhamana ya kutunza vyanzo vya maji ikiwemo maziwa hayo imetahadharisha wananchi kuendelea kuchukua hatua za uhifadhi wa vyanzo vyote vya maji na kuvilinda ipasavyo ili kupendezesha mji, kuweka mandhari nzuri, kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kuthibiti kuenea kwa jangwa ambako kunaweza kupelekea kupungua kwa vina vya maji.
Kaimu Afisa wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati, Danford Samson kwa niaba ya wizara alitoa angalizo hilo wakati wa kampeni hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada ya ofisi hiyo kuhakikisha kampeni ya kufanya Singida kuwa kijani inafanikiwa.
No comments:
Post a Comment