Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa. |
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB), Bw. Amos Cheptoo na kumhakikishia kuwa Tanzania itasimamia kikamilifu utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu yote inayopata fedha toka benki hiyo kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri Prof. Mbarawa amesema mazungumzo hayo yataongeza kasi ya utoaji fedha kutoka AfDB hasa kwa miradi ya viwanja vya ndege ambayo imechelewa kutokana na changamoto mbalimbali.
Ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kujengwa kupitia fedha za AfDB kuwa ni pamoja na barabara na viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania.
"Tumejipanga kuunganisha mikoa yote ya Tanzania na maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao kwa barabara za lami ili kukuza uchumu wa nchi," amesema Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB, Bw. Cheptoo amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha adhma ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa hususan barabara na viwanja vya ndege inatekelezeka.
Baadhi ya miradi hiyo ni barabara za Kabingo-Kasulu-Manyovu km 260.6 mkoani Kigoma, Mnivata-Newala-Masasi km 160 mkoani Mtwara na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato wa jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment