SERIKALI KUANZISHA MAKAZI YA WAZEE KIKANDA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 17 May 2022

SERIKALI KUANZISHA MAKAZI YA WAZEE KIKANDA

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula akizungumza na Wawakilishi wa viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka Mikoa ya Tanzania Bara katika Mkutano uliofanyika Mei 17, 2022 jijini Dodoma.

KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula amesema kuwa Wizara imepanga kuanzisha Makazi ya Wazee kikanda ili kuweka mazingira mazuri ya kuwalea Wazee wasiojiweza nchini.

Dkt. Chaula ameyasema hayo Mei 17, 2022 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka mikoa ya Tanzania Bara. Dkt. Chaula alisema kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kuwalea Wazee wasiojiweza na Ustawi wa Wazee kwa ujumla.

 

Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imejipanga kuanza kukarabati baadhi ya Makazi ya Wazee ili kuwezesha kuwa na Makazi hayo katika Kanda, hali itakayosaidia kuwa na Uratibu na huduma Bora zaidi kwa Wazee wasiojiweza chini.

 

"Hili ni muhimu sana na Wizara ipo katika mikakati ya kuboresha utoaji huduma katika Makazi ya Wazee inayoyaendesha kwa kuyaratibu kikanda ili kuwe na ufanisi na ubora katika huduma" alisema Dkt. Chaula.

 

Akizungumza baada ya ufunguzi wa Mkutano huo Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii anayeshughulikia masuala ya Wazee Tullo Masanja, alisema lengo la kuwakutanisha Wawakilishi wa viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka mikoa ya Tanzania Bara, ni kuwa mabalozi kwa wenzao katika kutoa maoni kuhusu Sera ya Wazee ili iwe jumuishi katika utoaji maoni kwa lengo la kuwa na Sera iliyo Bora.

 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Wazee David Lameck Sendo alisema Viongozi wa mabaraza ya Wazee Tanzania Bara wameamua kukutana ili kuweka mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha Usatwi wa Wazee ikiwemo kupitia rasimu ya maboresho ya Sera ya Wazee nchini na kutoa maoni yao katika Sera hiyo.

 

"Lingine la muhimu ni kuwa na Muongozo wa uendeshaji wa Mabaraza ya Wazee nchini kwani itasaidia kuwa na uelekeo sahihi na wenye tija katika kuendesha mabaraza hayo" alisema David Lameck Sendo.

 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Help Age Joseph Mbasha alisema Shirika hilo linashirikiana na Mitandao ya Wazee na Serikali katika kuhakikisha wanatoa rasilimali mbalimbali ili kusaidia jitihada za Serikali za kuwawezesha Wazee kupata huduma Bora katika Sekta mbalimbali ikiwemo Afya na kuwezesha Wazee hao kukutana kuzungumza na kujadiliana changamoto zao kupitia mabaraza ya Wazee.

 

Nao baadhi ya Wazee walisema Mkutano huo umekuja kwa wakati sahihi ambapo Wazee walio wengi amekuwa na matamanio ya kuwa na Sera itakayosaidia kuleta Ustawi wa Wazee nchini ikiwemo namna bora ya kuwatunza na kuwaenzi Wazee.

 

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii imewakutanisha Viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka mikoa ya Tanzania Bara kwa lengo la kuwapitisha katika masuala mbalimbali yahusiyo Ustawi wa Wazee nchini.

No comments:

Post a Comment