DKT. YONAZI ASEMA NENDENI MKATEKELEZE KWA VITENDO MAFUNZO MLIYOPEWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 23 January 2022

DKT. YONAZI ASEMA NENDENI MKATEKELEZE KWA VITENDO MAFUNZO MLIYOPEWA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza kwa njia ya mkutano mtandao (video conference) na wataalam kutoka Halmashauri mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu hao  ya utekelezaji wa anwani za makazi katika mkutano uliofanyika leo ofisi za TTCL, jijini Dodoma.

Na Prisca Ulomi, WHMTH, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amefunga mafunzo ya utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi kwa njia ya mkutano mtandao kwa wataalam wa Tanzania Bara na Zanzibar yaliyofanyika kwenye vituo vinne vya mkoa wa Mwanza, Mbeya, Tanga na Zanzibar.


Dkt. Yonazi amewataka wataalam hao 422 waliopatiwa mafunzo hayo ambapo wataalam 389 wametoka Tanzania Bara na 33 wametoka Zanzibar kwenda kutekeleza mafunzo hayo kwa vitendo kwa kuweka namba za nyumba, majina ya mitaa na barabara kwenye halmashauri wanazotoka ili kuhakikisha kuwa anwani za makazi zinatekelezwa nchi nzima na kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu.


Ameongeza kuwa utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi utasaidia kufungua kasi ya uchumi, utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi na kuifungua Tanzania kidijitali, “mwananchi yeyote atatambulika duniani na anaweza kufikiwa na mteja kwa ajili ya kuuza bidhaa au huduma, hivyo kila mwananchi awiwe kuwa na namba ya nyumba, jina la barabara au mtaa anapoishi,” amesema Dkt. Yonazi.


Pia, ametoa wito kwa kampuni, wadau mbali mbali na familia kuchangia utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi na kila mmoja awe balozi wa anwani za makazi na wataalam watoe taarifa kwa viongozi wao na Wizara iko tayari kuendelea kushirikiana kutekeleza hili.


Naye Mratibu wa Kitaifa wa Anwani za Makazi na Postikodi wa Wizara hiyo, Mhandisi Jampyion Mbugi, amesema kuwa wataalam waliopatiwa mafunzo hayo ni wataalam wawili kutoka kwenye kila halmashauri nchi nzima ambapo inahusisha wataalam wa TEHAMA, Ardhi, Mipango Miji na Ramani ambapo wamepatiwa mafunzo hayo kwa muda wa wiki moja kuanzia tarehe 17 Januari mwaka huu ya utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi ikiwemo kuweka namba za nyumba, jina la mtaa au barabara na kuweka taarifa za maeneo hayo kwenye mfumo wa kielektroniki wa NAPA ili anwani hizo zipatikane na kutumiwa na wananchi kwa kuwawezesha kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta.


Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wataalam wengine waliopatiwa mafunzo hayo, Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Kilindi, Tanga ndugu Anastius Biswalo Manumbu amesema kuwa wamepatiwa mafunzo hayo kwa vitendo na wataenda kuwafundisha wataalam wengine ili kuhakikisha kuwa anwani za makazi zinakamilika kwa wakati kuendana na azma ya Serikali na watazingatia miongozo iliyopo ya uwekaji wa anwani za makazi na postikodi.


Ufungaji huo wa mafunzo ya anwani za makazi na postikodi nchini, umehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vituo vinne ambapo mafunzo hayo yametolewa ikiwemo wawakilishi wa wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa mikoa ya Tanga, Mwanza, Mbeya na Zazibar ambapo kwa upande wa Zanzibar waliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ndugu Amour Bakari.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari


No comments:

Post a Comment