WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wanaosimamia miradi ya ujenzi waongeze kasi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwapa fursa wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Ametoa wito huo Januari 9, 2022 wakati akizungumza na mamia wa wakazi wa Jimbo la Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha afya cha shehia ya Kendwa ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za sherehe ya miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar.
"Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi na watendaji wanaosimamia mradi huu waendelee kushirikiana na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kukamilisha ujenzi huu kwa wakati uliopangwa ili kuwapa fursa wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar."
Pia amewataka viongozi wa shehia hiyo washirikiane na Wizara ya Afya kuhakikisha majengo na miundombinu iliyowekwa inatunzwa vema ikiwemo vifaa vitakavyonunuliwa sasa kwa matumizi ya sasa na baadaye.
Amewataka watumishi watakaopangiwa kuishi kwenye nyumba ya daktari wa kituo hicho, wayatunze majengo hayo lakini pia wapande miti na kutunza mazingira yanayowazunguka.
Akizungumzia uboreshaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kujenga vituo vingi zaidi ili wananchi wasiende umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
"Ninawasihi tuiunge mkono nia njema iliyoonyeshwa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi."
Waziri Mkuu ambaye kabla ya kuweka jiwe la msingi alikagua majengo matatu ya kituo hicho, amesema ameridhishwa na ujenzi wake na hasa kiwango cha ubora kilichopo.
"Nilipofika, nimekagua majengo kwenye zote kuanzia chini hadi juu. "Naipongeza kamati ya usimamizi wa ujenzi wa kituo hiki kwa kusimamia vizuri ujenzi wa kituo hiki. Ninaziagiza Kamati nyingine hapa nchini, ziige mfano wa Kamati hii ya Kendwa. Niliposikia fedha iliyotumika sikuamini. Fedha kidogo lakini imetoa majengo mazuri yenye viwango."
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho, Msimamizi Mkuu wa Majengo kutoka ZBA, Mhandisi Said Malik Said alisema ujenzi wa kituo hicho unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ulianza Agosti 28, mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Februari 27, mwaka huu.
"Gharama za ujenzi ni shilingi milioni 388 lakini hadi sasa zimetumika shilingi milioni 270. Kitakapokamilika, kituo kitakuwa na majengo ya OPD, maabara, chumba cha daktari, vyoo, chumba cha kumfanyia mgonjwa uchunguzi wa awali, chumba cha sindano na kufunga vidonda, kitengo cha meno, wodi ya akinamama wajawazito na nyumba ya daktari yenye uwezo wa kuchukua watumishi wawili kwa pamoja (2-in-1).
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga alisema kutokana na mabadiliko ya sheria, ujenzi wa kituo kama hicho utaendelea kwenye shehia zote.
Alisema kutokana na uhakiki wa walengwa wote uliofanyika Julai 2020 hadi Januari 2021, kaya 1,992 zilisema zinaishukuru Serikali na kwa hiyari yao, zikaamua kujitoa rasmi kwenye mpango wa TASAF wa kuhudumia kaya maskini.
"Kupitia uhakiki huo, kaya nyingine 211,800 zimekiri kuondokana na hali duni, na kwa hiyo, wako tayari kujitoa kwenye mpango huo baada ya miezi sita. Kutokana na uimarishaji lishe, afya na elimu, uandikishaji shuleni umeongezeka na mahudhurio pia yameongezeka."
Amesema watoto wengi waliosaidiwa na mpango huo, walipata matokeo mazuri ya ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu. "Matokeo yake, watoto 782 waliohitimu mwaka jana, wamechaguliwa kwenda vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini. Na hawa wamesaidiwa kupata ufadhili wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu," alisema.
Akielezea mafanikio mengine ya mradi huo, Bw. Mwamanga alisema waliwahimiza walengwa wa mradi huo kote nchini wawe wanatunza akiba kutokana na miradi wanayojishughulisha nayo. "Matokeo yake, vikundi 23,000 kutoka maeneo 71, vyenye wanachama zaidi ya 350,000 vimeweza kujiwekea akiba ya shilingi bilioni 6.9 ambapo miongoni mwao, vimeweza kukopeshana shilingi bilioni 2.6 ili waweze kushiriki shughuli za kiuchumi."
Hafla hiyo ya uwekaji jiwe la msingi ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Wilaya za Mkoani, ChakeChake, Wete na Micheweni, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wengine mbalimbali.
No comments:
Post a Comment