Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akiwa ziarani katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.
WITO umetolewa kwa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kuongeza wigo wa utekelezaji wa majukumu yake kwa kushirikisha zaidi jamii na kugusa maisha ya wananchi.
Akizungumza kwenye ziara ya kikazi aliyofanya katika Taasisi hiyo Januari 26, 2022, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Taasisi hiyo inafanya mambo mengi mazuri yanayofaa kuwa msaada kwa jamii.
Akikagua kazi za Kituo cha Kitaifa cha Utafiti na Uhifadhi wa Machapisho ya Wanawake (NWRDC), Dkt. Chaula ameonesha kuvutiwa na Miradi inayotekelezwa na kituo hicho ikiwemo program ya “Msichana Jasiri au She Brave” yenye lengo la kuwaimarisha mabinti wanafunzi katika vyuo na taasisi za elimu.
"Ili kufikia mafanikio ya program hiyo na nyingine ni lazima wananchi wanaohudumiwa kupatiwa taarifa na kujengewa uelewa wa mambo yanayowahusu". amesema Dkt. Chaula.
Dkt. Chaula amepongeza juhudi za Taasisi kwa kutambua, kulea na kukuza wanafunzi wenye mawazo ya kibunifu wakati wakukagua kazi za wabunifu wao, ikiwemo kutengeneza sabuni na dawa za usafi, biashara ya maharage mabichi, utengenezaji wa mafuta pamoja na bidhaa za urembo na mapambo.
Katika hatua nyingine wakati wa kukagua miradi ya ujenzi ya kumbi pacha za mihadhara na hosteli ya wasichana inayogharimu sh. bilioni 2.7; Dkt. Chaula amepongeza juhudi za Taasisi kusimamia vizuri miradi hiyo na kuhimiza ikamilike kwa wakati ili ianze kutumika.
Akiwa katika Ziara hiyo, Dkt. Chaula amefanya kikao na kuzungumza na watumishi wa Taasisi ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nafasi ya Katibu wa Wizara hiyo mnamo tarehe 08 Januari, 2022 na kuapishwa Ikulu ya Chamwino 10 Januari, 2022.
No comments:
Post a Comment