Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB, Dkt. Veronica Nyahende. |
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inatarajia kuanza kuwasajili 70,396 wanafunzi wanufaika wa mwaka wa kwanza katika mfumo wa kidigitali wa malipo ya fedha za mikopo ambao utawawezesha kupokea fedha ndani ya saa 24.
Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB, Dkt. Veronica Nyahende (pichani) amesema leo jumapili Januari 9, 2022, kuwa usajili huo utajumuisha kuchukuliwa kwa alama za vidole, taarifa za kibenki, picha pamoja na taarifa za usajili wa wanafunzi vyuoni.
Dkt. Nyahende amefafanua kuwa usajili huo utafanyika katika taasisi za elimu ya juu nchini kuanzia Jumatatu, Januari 10 hadi Februari 3 mwaka huu.
“Mfumo huu unaitwa ‘Digital Disbursement Solution’ maarufu kama DiDiS na tuliuanzisha mwaka 2018 ili kurahisisha fedha kuwafikia wanafunzi kutoka siku 10 hadi saa 24 hivi sasa,” amesema Dkt. Nyahende mwishoni mwa wiki.
Dkt. Nyahende amewakumbusha wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza ambao ni wanufaika wa mikopo na wengine ambao wamepata mikopo kwa mara ya kwanza mwaka 2021/2022 kujitokeza ili kusajiliwa.
“Malipo yote ya robo ya tatu kwa mwaka huu wa masomo yatafanyika kupitia mfumo huu, kwa hiyo ni muhimu kwa wanafunzi kujisajili ili wapokee malipo yao,” ameongeza Dkt. Nyahende.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyahende, maafisa wa HESLB watakuwa vyuoni kuanzia Jumatatu, Januari 10 ili kushirikiana na maafisa wa vyuo katika kazi ya usajili, na kuongeza kuwa taarifa za ziada kuhusu maeneo na muda wa usajili yatatolewa katika ofisi za maafisa mikopo wa vyuo husika.
Aidha Dkt. Nyahende ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za wanafunzi na maafisa mikopo katika vyuo kuwahamasiha wanafunzi wanufaika kujitokeza ili kujiandaa kupokea fedha za malipo ya mikopo bila usumbufu.
“Usajili huu ukifanikiwa, maafisa mikopo wataondokana na usumbufu wa kutunza kumbukumbu kwa karatasi na wanafunzi watakuwa wanapokea fedha haraka na hivyo kutumia muda mwingi kusoma” amesisitiza Dkt. Nyahende.
HESLB ilianzishwa kupitia Sheria ya HESLB (SURA 178) ya mwaka 2004 ikiwa na
jukumu la kutoa mikopo au ruzuku kwa wanafunzi wahitaji na kusimamia urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga TZS 570 bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na zinazowanufaisha jumla ya wanafunzi 168,000.
No comments:
Post a Comment