DARAJA LA TANZANITE KUANZA KUTUMIKA FEBRUARY MOSI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 31 January 2022

DARAJA LA TANZANITE KUANZA KUTUMIKA FEBRUARY MOSI

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu (Sekta ya Ujenzi), Mha. Balozi Aisha Amour, alipokagua Daraja jipya la Selander (Tanzanite), lililokamilika ujenzi wake kwa asilimia 100 na kuanza kutumika rasmi Februari mosi, 2022, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mha. Rogatius Mativila.

Muonekano wa Daraja jipya la Selander (Tanzanite) ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutumika rasmi Februari 01, 2022, jijini Dar esa Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mha. Balozi Aisha Amour, akitoa maelekezo wa uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), alipotembelea Daraja jipya la Selander (Tanzanite), jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mha. Rogatius Mativila (kushoto), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati alipokagua Daraja jipya la Selander  (Tanzanite) lililokamika ujenzi wake kwa asilimia 100 na kuanza kutumika rasmi Februari 01, 2022 jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameeleza kuwa magari yataruhusiwa kupita katika Daraja la jipya la Selander (Tanzanite), kuanzia tarehe mosi mwezi Februari, 2022 mara baada ya ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 100.

Ameongeza kuwa daraja hili litaruhusiwa kwa wananchi kulitumia bila malipo kwa masaa 24 kwa siku.


Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.30 na barabara unganishi kilomita 5.2 lililogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 243.


“Daraja hili ni muhimu sana kwa sababu litapunguza changamoto ya foleni sababu daraja la zamani la Selanda lilikuwa limeshazidiwa na wingi wa magari hivyo kukamilika kwake ni muarobaini kwa  foleni za jiji la Dar es Salaam”, amesema Prof. Mbarawa.


Waziri Prof. Mbarawa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kutoa fedha za ujenzi na matengenezo ya miundombinu nchini ili Tanzania kufunguka zaidi katika miundombinu yake na hivyo kuchochea uchumi wa Taifa.


Aidha, Prof.Mbarawa amewataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha wanaweka alama zote muhimu za barabarani katika maeneo yote ili kuongoza vizuri watumiaji wa barabara na kupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika.


Vilevile amewaagiza Mameneja wote TANROADS nchini kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ili kuhakikisha inakuwa salama na  kupitika wakati wote hasa hasa katika madaraja ili kuyakinga kutopata athari za mvua zinazoendelea kunyesha.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Balozi Aisha Amour, amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha miundombinu ya barabara na madaraja inatunzwa na kusimamiwa kwa karibu ili kuzingatia thamani ya fedha.


Balozi Aisha, ametoa wito kwa wananchi wote wanaotumia miundombinu ya barabara kuhakikisha wanatumia kwa matumizi sahihi waliyoweka kwa kufata taratibu zote.


“Nitoe wito kwa wananchi na watumiaji vyombo vya moto kufuata matumizi sahihi ya alama na kwa madereva wapaki maeneo ya maegesho waliyowekea ili kusaidia kupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika”, amesisitiza Mha. Balozi Aisha.


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS Mhandisi Rogatius Mativila, amemueleza Waziri huyo kuwa daraja mpaka sasa limekamilika kwa asilimia 100 na zoezi la kupitisha magari litaanza saa 12 asubuhi.


Mativila ametoa rai kwa watumiaji wa daraja hilo kuwa waangalifu na kuzingatia alama mbalimbali zilizowekwa ili kuepusha ajali.


Daraja jipa la Selander (Tanzanite) ni mojawapo ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka katika jiji la Dar es Salaam.


(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)


No comments:

Post a Comment